MAONI: Ufisadi unaoendelezwa na magavana katika kaunti unahujumu matunda ya ugatuzi
HUKU tukiendelea kulaumu hatua ya Serikali ya Kitaifa kwa kuchelewesha fedha kufikia Serikali za Kaunti kwa wakati ufaao, na kuwa kizingiti kwa magavana kufanikisha mikakati ya maendeleo mashinani, visa vya ufujaji wa pesa za umma vinaendelea kufichuliwa katika kaunti nyingi nchini na magavana pia wamenaswa katika mitego ya ufisadi kwa ushirikano na baadhi ya maafisa wao.
Visa vya ufisadi vinafaa kumalizwa katika kaunti zetu ili raia wavune matunda ya ugatuzi bila unyanyasaji unaoendelea katika kaunti.
Kinachovunja moyo ni kutambua kuwa baadhi ya miradi iliyoanzishwa na kutengewa fedha imekwama tangu ujio wa ugatuzi na iliyokamilika nayo ilifanywa kwa njia isiyofaa.
Kiwango kikubwa cha fedha ambao ni ushuru wetu kimepotea kupitia ufujaji na magavana wanafaa kuwajibikia kosa hilo.
Ili kulinda raslimali zetu na kufurahia mafanikio ya ugatuzi, lazima raia wachague viongozi wenye maono ya kuimarisha huduma za afya, elimu, maji, miundomsingi, kilimo na kufanikisha miradi endelevu mashinani.
Baadhi ya magavana wamefeli na wanafaa kujua ukweli kwamba, maono yao hayasaidii tena ugatuzi. Mfano, katika Kaunti ya Taita Taveta, wagonjwa wanapotembelea Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi, wanakosa huduma muhimu kama vile MRI, X-ray, oksijeni na mashine za kufanyia uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
Maskini anapokosa matibabu katika hospitali za umma kama vile ya Moi mjini Voi, anarudi nyumbani na maradhi yake ambapo anateseka au hata kufa. Je, raia kama huyo kweli anajua mafanikio ya ugatuzi nchini?
Ndiyo maana hata raia hawajitokezi kushinikiza Hazina ya Kitaifa kuharakisha uwasilishaji wa pesa kwa kaunti kwa wakati unaofaa. Ikiwa magavana watafeli kubadilisha mazingira, uchumi na ustawi katika kaunti zao, basi raia mashinani watakosa kujivunia ugatuzi.
Wanaoshiriki ufisadi na kutatiza mipango ya maendeleo mashinani wanafaa kuadhibiwa vikali. Itakuwa onyo zuri maana baadhi ya maafisa waliohusishwa na ufisadi katika serikali ya kwanza ya ugatuzi na ya pili wangali huru wakiendeleza utajiri wao kwa pesa walizopora.
Mtindo huo ndio umewapa msukumo viongozi wa sasa kuendelea kupora na kuumiza ugatuzi bila huruma.