Vijana wa Mlimani wasikubali wanasiasa kuwatumia visivyo
KATIKA siku za hivi majuzi, kumeibuka mkondo wa kuhofisha ambapo makundi ya vijana yametumika kuzua vurugu katika mikutano ya kisiasa.
Matukio haya yamejitokeza bayana katika eneo la Mlima Kenya huku pande hasimu zikirushiana cheche za maneno na kulaumiana kwa kuwatumia vijana kusababisha vurugu na kuwashambulia viongozi. Ghasia zilizogeuza hafla ya maombi kuwa uga wa fujo eneo la Shamata, Nyandarua, ni mfumo wa matukio hayo.
Huku wandani wa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua wakielezea wasiwasi wao kuhusu usalama wake, viongozi wanaoegemea chama tawala cha UDA wamepuuzilia mbali suala hilo wakilitaja kama “njama za kuvutia huruma kutoka kwa raia.”
Viongozi serikalini nao wamemsuta vikali Bw Gachagua wakimshutumu pamoja na wandani wake, kwa kuchochea vijana kushiriki alichotaja kama “siasa chafu” kwa maslahi ya kibinafsi.
Huku haya yakijiri, aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga, aliyesababisha taharuki kote eneo hilo miaka michache iliyopita, ametangaza vita kumdhibiti Bw Gachagua.
Matukio yote haya yanaashiria mustakabali wa kuhofisha kwa vijana katika Mlima Kenya ikizingatiwa fahali wawili wanapopigana nyasi ndizo huumia.
Inasikitisha katika enzi hii baadhi ya viongozi bado wanatumia vijana kufanikisha azma zao za kibinafsi.Katika kizazi hiki cha maendeleo kiteknolojia na kiutandawazi ambayo yamezua mwamko mpya, ingetarajiwa kuwa vijana hawatakubali kushikwa mateka na watu wanaofahamu vyema hawawajali.
Huenda tusiwalaumu vijana sana kwa sababu wengi wao wamekata tamaa maishani kwa kukosa kazi au namna ya kujikimu kimaisha.
Ili kutuliza mawazo na kujaribu kusonga mbele, baadhi wamegeukia matumizi ya mihadarati na unywaji pombe haramu zinazosambazwa na mabwanyenye wenye ushawishi mkubwa.
Viongozi wenye mazoea ya kuwatumia vijana vibaya wanafahamu fika udhaifu wao wanaoutumia kulipiza kisasi kwa mahasimu wao kupitia vijana.
Kwa sababu ya kupumbazwa au kukosa matumaini maishani, baadhi ya vijana kutoka Mlima Kenya na maeneo mengine nchini wameishia kukubali chochote wanachoagizwa kufanya ilmradi walipwe.
Matokeo yake ni maisha ya vijana kuharibiwa kupitia kulemazwa, kufungwa jela na vifo vya mapema huku wakiacha familia zao kwa majonzi pasipo mfariji.
Katika jamii iliyostaarabika, viongozi wangekuwa wanajishughulisha na kubuni mikakati ya kuboresha taasisi za elimu, vituo vya kiufundi na muhimu zaidi, kuunda nafasi za ajira kwa vijana.