Wanatawala nyumba yangu! Ni msimu wa wazazi kulalamika likizo ndefu ikianza
UMEWADIA ule msimu wa wazazi kuanza kulalamika kama watoto. Kuhusu nini? Uwepo wa watoto wao nyumbani wakati wa likizo ndefu. Watoto hawaendi shuleni mpaka Januari!
Mara ‘wanakula chakula changu’; mara ‘runinga si yangu tena’; mara ‘wananipigia kelele’; mara ‘wanatawala nyumba yangu’; mara ‘wanacheza michezo hatari’; mara ‘wamenichafulia nyumba’; mara ‘sasa watakaa nyumbani na nani’; mara ‘hawa watoto hawana adabu!’
Hivi tunazungumzia watoto wa nani? Wa jirani, au wako mwenyewe? Wa kukopa, au wa kuzaa? Wa kuokotwa, au uliobeba miezi 9 tumboni, mwishowe wakatua duniani, ukafurahi na kumshukuru Mungu kwa kukuondolea aibu ya utasa na ugumba?
Unataka wale chakula cha nani? Mbona unageuka mchoyo? Unataka wakatazame runinga kwa jirani ilhali ulinunua kiwambo kikubwa cha familia? Mbona unakuwa mnoko hivi?
Kimya unachokitaka hakipatikani katika mazingira ya watoto au vijana wanaokua, hivyo labda utafute kwa kwenda kupunga upepo, hela zikikukataa ujifungie chumbani na kujilaumu kwa kubuni ‘tatizo’ unalolalamikia.
Huko unakoteta kwamba wanatawala ni kwao pia, tena wewe mwenyewe ndiwe uliyewaambia ni kwao, ukajitambulisha kama mzazi wao, sikwambii uliwaleta duniani bila kwanza kushauriana nao, angaa kuwauliza iwapo waliridhia kuzaliwa.
Kuhusu michezo yao hatari inayokuudhi nusra ikupe msongo wa mawazo, hujui wamerithi kwako? Umesahau ulivyojaribu kushindana na nyani kuruka kutoka mti mmoja hadi mwingine, ukakosa tawi, ukapiga chini kwa mshindo na kuzimia?
Hebu kwanza ushukuru upepo wa Mungu uliokufufua, ukatia akili usiwahi kuigiza nyani tena, ukaishi mpaka leo kutuhadithia kuhusu masaibu yako utotoni.
Usilalamike eti wanakuchafulia nyumba. Wape fagio wafagie kutoka ndani hadi nje ya nyumba kisha wachome takataka hizo. Mfunze mtoto kupiga deki sawasawa mpaka ajue thamani ya usafi na unadhifu. Mbona unalea vibaya kisha unalalamika?
Ikiwa huwaamini kiasi cha kuwaacha nyumbani peke yao ukienda kwa shughuli za kutwa, basi buni nafasi ya kazi kwa kumwajiri yaya kimya-kimya. Uliwazaa ukijua malezi ni gharama.
Eti hawana adabu? Wewe unayo? Aliyefaa kuwafunza adabu ni nani? Ama labda wewe ni mmoja wa wazazi ambao huamini kumfunza mtoto nidhamu ni jukumu la mwalimu?
Mwalimu mwenyewe ana watoto wake anaopaswa kufundisha nidhamu, tena yeye si yaya wako akulelee mtoto, hivyo acha kukimbia majukumu uliyojiletea mwenyewe ulipoamua kuwa mzazi. Huwezi kustaafu wala kwenda likizo ya malezi, ni kazi ya kufululiza.
Ikiwa wewe ni mtoto, na umesoma makala hii, lazima utumie akili. Kwa usalama wako, usithubutu kumtishia mzazi wako kwa mambo uliyosoma hapa. Mimi pekee ndimi niliye na uhuru wa kuyasema mbele ya wazazi wenzangu bila kuogopa kutiwa adabu.