Maoni

Wetang’ula atajuta akipuuza vitisho vya kumng’oa kama spika bungeni

Na BENSON MATHEKA February 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula hafai kuchukulia vitisho vya kuondolewa kwake ofisini kama mzaha hasa baada ya kupuuza uamuzi wa mahakama uliosema alikiuka Katiba kwa kutangaza Kenya Kwanza muungano wa walio wengi.

Vitisho hivyo vilivyoanza mwaka jana baada ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuanza ukuruba wake na Rais William Ruto viliibuka tena wiki hii na hii inafaa kumtia baridi Bw Wetang’ula aanze na kung’amua kwamba, mawimbi ya siasa yameanza kumpiga.

Sio kwamba seneta huyo wa zamani wa Bungoma hajui kwamba Azimio ina wabunge wengi, lakini yeye ni mateka wa serikali kuu ambayo inahisi hatari iwapo itachukua mrengo wa walio wachache.

Kwa hili, Bw Wetang’ula anatumiwa kulinda maslahi ya Rais William Ruto ambaye ataonekana kupoteza iwapo Kenya Kwanza utakuwa muungano wa wachache.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula anapaswa kusoma dalili za wakati na kujifunza kutoka kwa masaibu ya aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ambaye licha ya kumsaidia Rais Ruto wakati wa kampeni hadi akaingia mamlakani, alihakikisha ameng’olewa bila huruma.

Akiwa Spika, Bw Wetang’ula alitumiwa kufanikisha kuondolewa kwa Gachagua na anaonekana kusahau kwamba, ni ODM iliyosaidia Kenya Kwanza kupata wabunge wa kutosha wakati wa mchakato huo.

Kwa kuwa ODM inamezea mate viti vya upande wa walio wengi na awali ilielezea azma ya kutwaa kiti cha spika kuimarisha ushirikiano wake na serikali, na ikizingatiwa muungano wa Kenya Kwanza unafifia baada ya vyama vya Amani National Congress (ANC) na United Democratic Alliance (UDA) kuungana, na kwamba amekataa chama chake cha Ford Kenya kufuata mkondo wa ANC, Wetang’ula anafaa kufahamu kuwa huenda siku zake katika kiti cha Spika zimehesabiwa na njia bora ya kujinusuru kwa heshima ni kuondoka kabla afurushwe kupitia kura.