Habari Mseto

Masaibu ya Arati: ODM yataka hatua kali dhidi ya Osoro, polisi

January 12th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) sasa kinaitaka Mamlaka Inayosimamia Utendakazi wa Polisi (Ipoa) kuchunguza vurugu zilizotokea Jumatatu wiki hii katika Kaunti ya Kisii ambapo watu wanne walijeruhiwa kwa risasi.

Fujo hizo zilitokea Nyakembene, eneobunge la Mugirango Kusini pale Gavana wa Kisii Simba Arati na mbunge wa eneo hilo Silvanus Osoro walikorofishana.

Inadaiwa wafuasi wa Bw Osoro ndio waliofyatua risasi zilizotawanya waliokuwa wamejitokeza kusikiliza hotuba ya gavana Arati.

Lakini Bw Osoro ambaye pia ni kiranja wa wengi katika Bunge la Kitaifa, amekanusha madai hayo.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema Ijumaa akiwa mjini Kisii kwamba watu waliofyatua risasi hizo walikuwa ni maafisa wa polisi walioandamana na Bw Osoro.

Alisema hayo kwenye ziara ya kuonyesha mshikamano na Bw Arati, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho cha Chungwa.

Bw Sifuna ambaye ni Seneta wa Nairobi, alisema wana ushahidi wa kutosha kuwa baadhi ya maafisa hao walitoka jijini Nairobi na aliwataja majina yao hadhrani na nambari zao za usajili kikosini.

Pia alimkemea Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki na Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kwa kutolizungumzia tukio hilo.

Bw Sifuna alisema Bw Osoro anafaa kushinikizwa kuandikisha taarifa cha kile anachokijua kuhusiana na fujo hizo.

“Bw Osoro anafaa kurekodi taarifa ikiwa hawezi kukamatwa,” Sifuna, alisema, huku pia akiongeza kwamba kamanda wa polisi wa Kisii Charles Kases anafaa kuhamishwa.

Seneta Sifuna aliwatambua maafisa aliodai walifyatua risasi hizo kama Kevin Lagat, Peter Muge, na Simon Muriithi walio katika kituo cha polisi cha Nyanchwa, kaunti ndogo ya Kitutu ya Kati.

“Lagat amehamishwa hadi kituo cha Polisi cha Bunge tangu tukio hilo,” Bw Sifuna akadai.

Katibu huyo alisema afisa mwingine, Maurice Kiambi alisafirishwa kutoka kituo cha polisi cha Langata kushiriki ufyatuaji huo.

Bw Sifuna alisikitishwa kuwa hadi sasa, hakuna hata mshukiwa mmoja aliyetiwa mbaroni na akaitaka Ipoa itoe majibu yake ndani ya wiki mbili.