Habari za KitaifaMakala

Masengeli motoni iwapo atapuuza maagizo ya korti mara ya saba

Na RICHARD MUNGUTI September 8th, 2024 3 min read

KAIMU Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli anatarajiwa kufika katika mahakama kuu Jumatatu Septemba 9,2024 kueleza waliko wanaume watatu waliotoweka Agosti 19,2024 mjini Kitengela Kaunti ya Kajiado.

Mahakama kuu ilimuahidi Bw Masengeli kwamba atakumbana na makali ya sheria anayotekeleza kwa kutofika kortini mara sita (6).

Jaji Lawrence Mugambi alisema kwamba Masengeli amedharau mahakama na kukaidi maagizo ya kufika kortini mara sita kati Agosti 23 hadi Septemba 5,2024.

“Bw Masengeli hakuona umuhimu wa kufika kortini kueleza kuhusu maisha ya Wakenya watatu waliotoweka Agosti 19,2024 na kufikia leo hawajulikani waliko,” Jaji Mugambi alisema huku “akimwagiza IG huyo afike kortini Septemba 9,2024.”

Jaji huyo alisema Masengeli hajaona manufaa ya kufika kortini kueleza waliko watatu na anatakiwa kuomba msamaha kwa kukaidi maagizo ya korti.

Badala ya kufika kortini Septemba kama alivyoagizwa, aliwatuma mawakili wa Serikali Charles Mutinda na Wanjiku Mwangi kueleza “hayuko Nairobi na kwamba yuko Mombasa kikazi.”

Kaimu IG huyu aliamriwa na Jaji Mugambi Agosti 23, 2024 awafikishe kortini mwanaharakati Bob Micheni Njagi na ndugu wawili Jamil Longton na Nadim Hamed Longton waliotekwa nyara Agosti 19,2024.

Bw Masengeli alikosa kufika kortini kueleza waliko mwanaharakati huyu na ndugu hao wawili waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa polisi.

“Familia za watatu hawa hazijui waliko. Wametafutwa katika Mochari na  hospitali na hawajapatikana. Familia za watatu hao zinafikiria walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi na tangu wakamatwe hawajashtakiwa na wala hawajulikani waliko,” Jaji Mugambi alifahamishwa.

Jaji Mugambi alimwamuru Bw Masengeli afike kortini aeleze waliko watatu hao akisema ni “jukumu la kulinda maisha na mali ya wananchi.”

Jaji huyo alisema Ijumaa (Septemba 5 2024) kwamba ni jambo la kushangaza sana badala ya Bw Masengeli kufika kortini kueleza waliko wanaume hao watatu alichagua kuhudhuria warsha.

“Bw Masengeli amepuuza maagizo ya mahakama hii. Aliona ni bora kuhudhuria warsha ya masuala ya usalama iliyowajumuisha maafisa wakuu kitengo cha usalama kutoka kaunti za Mombasa, Lamu , Mandera, Garissa na Isiolo badala ya kufika kortini kueleza waliko Njagi, Nadim na Aslam,” alisema Jaji Mugambi.

Jaji huyo alisema maisha ya binadamu ni ya thamani kuu na sharti Bw Masengeli afike kortini kueleza waliko watatu hao.

Chama cha Mawakili Nchini (LSK) kupitia kwa rais wake Faith Odhiambo na mawakili wa familia za watatu hao waliotoweka walimsihi Jaji Mugambi amwadhibu vikali Bw Masengeli.

Maafisa mapuuza

“Bw Masengeli amejiunga na kundi la maafisa wakuu serikalini wanaokaidi, kupuuza na kudharau mahakama pamoja na maagizo yake. Endapo mahakama hii haitamwadhibu Bw Masengeli basi maagizo ya mahakama yatachukuliwa hayana maana,” wakili Hosea Manwa alimweleza Jaji Mugambi.

Bw Manwa aliambia korti “wakati ni sasa adhabu kali itolewe kwa Masengeli ili maafisa wakuu serikalini wanaokaidi maagizo ya mahakama wapate funzo.”

Chama cha mawakili nchini (LSK) kupitia rais wake Faith Odhiambo na Bw Manwa kiliwashtaki IG, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Idara ya Ujasusi (NIS) kikiomba asasi hizi za serikali ziagizwe ziwafikishe kortini wanaume hao watatu waliodaiwa walikuwa wanahamasisha wanarika kushiriki katika maandamano ya Gen Z eneo la Kitengela kupinga sera za utawala wa serikali ya Rais William Ruto.

Lakini Bw Mutinda (wakili wa serikali) alijaribu kumtetea Bw Masengeli lakini mahakama ikamzima kwa kumtaka IG afike kortini kuomba msamaha na kuadhibiwa kabla ya kesi kuendelea.

“Hii kesi haitasikizwa hadi pale Masengeli atakapofika kortini na kuomba msamaha na kutii maagizo ya korti ya kueleza waliko ndugu hao wawili na mwanaharakati Njagi,” Jaji Mugambi alisisitiza.

Bw Manwa alimkumbusha Jaji Mugambi kwamba maafisa wakuu wa polisi hapo awali na aliyekuwa Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i walikaidi agizo la mahakama na kumfurusha mwanaharakati Miguna Miguna.

Pia LSK ilisema kuwa hivi  majuzi polisi wameagizwa wasiwanyunyizie maji ya rangi na kuwarushia vitoa machozii waandamanaji lakini hawakutii.

Pia Jaji Mugambi alielezwa mahakama kuu iliamuru polisi wasiwateke nyara waandamanaji pamoja na kuwapiga risasi waandamanaji lakini wakakaidi maagizo ya mahakama kuu.

Kila mmoja nchini anasubiri kwa hamu na ghamu kuona hatua atakayochukuliwa Masengeli.

Je mahakama itatumia ngeli ipi kumwadhibu Bw Masengeli, kaimu IG.

[email protected]