Makala

Mashoga wataka watengewe wadi maalum hospitalini wakiugua  

January 28th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

MASHOGA wa Murang’a wameomba serikali ya Kaunti iwatengee wadi maalum za kulazwa wakiponesha majeraha na pia wawekwe katika mpango wa kliniki za bure mashinani.

Mshirikishi wa masilahi yao eneo hilo Bw Gregory Ndung’u, 38, alisema Mjini Kiria-ini mnamo Januari 28, 2024 kuwa wametengwa katika huduma za kimsingi.

“Kwa demokrasia, haki na uwazi hata tunafaa kupewa asilimia fulani ya serikali ya Gavana Irungu Kang’ata kwa kuwa hatufai kubaguliwa. Lakini kwa kuwa huwa tumetengwa na kuvishwa nembo za aibu, hatujaafikia viwango vya kudai kipande cha utawala serikalini,” akasema.

Bw Ndung’u aliongeza kwamba “kwa sasa hata hatuwezi tukajitokeza hadharani kudai haki zetu au kuuza sera zetu kwa kuwa hata tunaweza tukauawa”.

Hata hivyo, aliongeza kwamba “huwa tuna ufuasi kwa kuwa katika Kaunti ya Murang’a pekee tuna wanachama 3, 000”.

Alisema wanachama hao hukutana na changamoto nyingi katika hali zao za kupendana.

“Janga kuu ni la kiafya ambapo tukipata majeraha ama maambukizi huwa tunaogopa kufika hospitalini kwa kuwa wengi wa wauguzi hawatuelewi,” akasema.

Baadhi ya majeraha ambayo wao hukumbana nayo, akasema, ni “pamoja na kuraruka, kukwaruzwa au kuambukizwa maradhi ya zinaa”.

Bw Ndung’u aliteta kwamba “hata sisi huwa tunadhulumiwa kimapenzi na washirika wetu na kuishia kuhitaji huduma za dharura za kimatibabu”.

Alisema kwamba “tukifika hospitalini tukiwa na majeraha huwa tunakejeliwa vibaya sana huku wengine hata wakitupiga picha na kuzipachika katika mitandao ya kijamii”.

Aidha, alisema kwamba “tuna washirika wetu katika afisi kubwakubwa huku Murang’a, lakini hatuwezi tukawataja kwa kuwa watatuua”.

[email protected]