Habari Mseto

Maskwota wataka kugawia Ngilu ardhi ‘waishi kwa amani’

May 11th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MASKWOTA wanaozozana na familia ya aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu kuhusu umiliki wa ardhi mjini Mombasa wamesema wako tayari kumgawia mwanasiasa huyo sehemu katika eneo hilo.

Bw Mwijuma Mbwana na Bw Njira Ngala wamesema wako tayari kuishi kwa amani na familia ya Bi Ngilu katika ardhi hiyo.

“Sisi hatuna shida, tutamkaribisha na tumgawie sehemu ya kujisitiri na familia yake,” waliambia Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi Lucas Naikuni.

Watu hao wamelilia mahakama kuwa hawana mahali pa kwenda kwani wamekaa katika ardhi hiyo tangu utotoni.

Mbwana na Ngala waliambia mahakama kuwa wamejenga nyumba zao katika ardhi hiyo na kuwa sehemu hiyo imekuwa nyumbani kwao tangu kuzaliwa zaidi ya miaka 30 iliyopita.

“Hatuna fedha ambazo tunaweza kutumia kununua ardhi nyingine, tunaomba mahakama ituonee huruma na itutendee haki. Sisi ni Wakenya na haitakuwa vyema kufurushwa kwenye eneo ambalo tumekulia tangu utotoni,” walisema.

Mawili hao ni miongoni wa watu zaidi ya 19 ambao Bi Ngilu amewashtaki kwa kuvamia ardhi ya familia yake.

Vile vile, maskwota wameiomba mahakama kuzingatia masaibu yao iwapo itabaini kwamba stakabadhi za umiliki wa Bi Ngilu ni za kweli.

“Sina uhakika kama ardhi hiyo ina hatimiliki, na ikiwa iko, basi mahakama inapaswa kuchunguza jinsi ilipatikana. Ikiwa hatimiliki alizonazo mlalamishi ni za kweli, basi naiomba mahakama hii itusaidie kutafuta mahali pengine pa kuishi. Sisi ni Wakenya na tunastahili mahali pa kuita nyumbani,” akasema Bw Omar Kai.

Kupitia kwa wakili wao Hamisi Salim, maskwota hao wanataka mahakama isiwaondoe katika ardhi hiyo kwa madai kuwa wameishi humo tangu mwaka wa 1970.

Maskwota hao wamekanusha madai kuwa ardhi hiyo ni ya Bi Ngilu au kuwa ana haki ya kunufaika.

“Tunaamini kwamba hati za umiliki ya ardhi husika zilipatikana kwa njia ya ulaghai na au kwa njia ya kupotosha hivyo tunataka zifutiliwe mbali,” walisema.

Baadhi ya maskwota wanadai kuwa wamekaa kwenye ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka 20, huku wengine wakihoji kuwa wamejenga majengo hapo baada ya kukaribishwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa Bi Ngilu aliwasilisha kesi hiyo mwaka wa 2022 pamoja na Lunde Jemi Mwendwa, Mwende Kathetia na Syalo Ngilu Mwendwa.

Wanne hao waliwasilisha kesi hiyo kama wawakilishi wa kibinafsi wa mali ya marehemu Michael Mwendwa Ngilu.

Hata hivyo, Bi Ngilu aliiambia mahakama kwamba alichukua umiliki wa mali hiyo kama mwakilishi wa kibinafsi wa marehemu mumewe.

“Siku zote tumekuwa tukimiliki mali hiyo kwa amani bila kusumbuliwa baada ya kupata hati muhimu,” alisema.

Bi Ngilu aliwasilisha stakabadhi za kuthibitisha kuwa alipewa idhini ya kuridhi ardhi hiyo.

Ardhi hiyo iko karibu na Almashauri ya Bandari nchini na karibu na barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.

Mwanasiasa huyo alienda mahakamani mwaka wa 2022 alipopata habari kuhusu kuvamiwa kwa mali yao na watu wasiojulikana.

Alilalamikia mahakama kwamba washtakiwa wanaendelea kumiliki mali hiyo kinyume cha sheria, hivyo kuzuia maendeleo au manufaa yoyote kutoka kwayo.

Bi Ngilu alifahamisha mahakama kuwa juhudi kadhaa za kuwataka washtakiwa kuondoka katika ardhi hiyo zimekabiliwa na upinzani, dhuluma na ghasia.

Mnamo Oktoba 2022, korti ilitoa maagizo ya muda ikisema kwamba hakuna ujenzi zaidi unapaswa kufanywa kwenye eneo hilo.