Makala

MATHEKA: Serikali isipuuze ripoti za njaa kukumba maeneo

August 14th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Ukame umeanza kubisha hodi katika baadhi ya maeneo nchini. Maelfu ya Wakenya wanakabiliwa na hatari ya kufa njaa huku bei ya bidhaa za chakula zikiendelea kupanda.

Mifugo wameanza kuangamia na wafugaji wanalazimika kuwauza kwa bei ya kutupa ili wasipate hasara zaidi.

Kwa miaka mingi, hali hii imekuwa ikikumba nchi yetu na ajabu ni kuwa huwa inatumiwa kutimiza malengo ya kisiasa badala ya kuokoa maisha ya wanaokufa njaa.

Kwa sababu kaunti kame zinajulikana na kuna serikali inayofanya kazi nchini, hakuna haja ya kusubiri hadi wanahabari waangazie habari za watu wanaokufa njaa ili hatua zichukuliwe.

Hakuna afisa wa serikali asiyejua kwamba wakazi wa Turkana, Baringo, Wajir, Tana River, Garissa, Mandera na Kwale wanakabiliwa na njaa.

Majuzi, vita vilizuka kati ya wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta na wafugaji kutoka Kaunti ya Tana River hadi mtu mmoja na ngamia zaidi ya 20 wakauawa kwenye mzozo wa malisho.

Kwa sababu ya ukame, visa vya wanyama pori kutoroka mbuga na kuwaua watu vimeripotiwa maeneo tofauti nchini.

Hii inaonyesha hatari inayosababishwa na kiangazi hatua zikikosa kuchukuliwa mapema.

Nina hakika kwamba serikali ina uwezo wa kukabili hali hii kwa kununua chakula kutoka maeneo ambayo kwa kawaida hupata mvua ya kutosha na kukipeleka maeneo ambayo hukumbwa na kiangazi.

Nina hakika serikali ina uwezo wa kuhakikisha kila eneo kote nchini linapata maji ya kutosha wakati wa kiangazi.

Maeneo hayo yako katika nchi moja na serikali moja na inashangaza kuona serikali ikisubiri hadi watu wafe njaa ili ianze kushughulika. Hii ni aibu kubwa kwa serikali iliyo na idara ya kukabiliana na majanga na mikasa.

Wizara za maji, kilimo, afya, ugatuzi na usalama wa kitaifa zina uwezo wa kuzuia Wakenya kufa njaa kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo wanahabari wataifahamu wakati wa utekelezaji wake.

Wizara hizi zinatengewa mabilioni ya pesa na haziwezi kuepuka inapasa kutoa misaada ya chakula, dawa na maji kwa wakazi wa maeneo yanayokumbwa na ukame.

Pia inafaa kuwasaidia wafugaji kwa kununua mifugo wao na machifu watoe habari sahihi kwa idara husika, wasiuze chakula cha misaada na kwamba chakula hicho kitatolewa bila ubaguzi kwa kila Mkenya anayekabiliwa na njaa.