Makala

Mazoea kuiba divai ya babake kasisi yalivyomgeuza gwiji wa pombe

March 26th, 2024 2 min read

DOMNIC OMBOK NA WANDERI KAMAU

SAFARI ya Bw Godfrey Ochola kukabiliana na uraibu wa pombe ilianza bado akiwa mtoto.

Akiwa mchanga, alikuwa na mazoea ya kuiba divai ya babake na kuonja kiasi kidogo.

Babake alikuwa kasisi katika Kanisa la Kianglikana (ACK) huku yeye (Ochola), akihudumu kama mmoja wa vijana kumsaidia kasisi.

“Nilianza kuonja pombe nikiwa katika shule ya upili mwaka wa 1995. Babangu alikuwa kasisi katika kanisa la ACK, hivyo nilihudumu pamoja na yeye,” akaeleza.

“Kama kijana aliyekuwa msaidizi wa kasisi, ningeonja divai kwa kiwango kidogo. Ningeichanganya kwa maji ili kutonuka. Hata hivyo, babangu alinipata,” akasema.

Uraibu wa Bw Ochola ulidorora, baada yake kuanza kunywa pombe aina ya chang’aa.

Uraibu wake ulimfanya kuacha masomo yake katika Chuo cha Mafunzo ya Kiufundi cha Kisumu.

Hilo pia lilimfanya kuacha kazi alizokuwa akipata, hata zile alizokuwa akitafutiwa na babake.

Licha ya miaka mingi aliyokuwa amezama kwenye ulevi, ni hadi 2019 alipoamua kuchukua hatua ya kubadilisha mkondo wa maisha yake, kwa kuachana na matumizi ya vileo.

Alijipeleka katika afisi za Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabliana na Matumizi ya Mihadarati (NACADA) jijini Kisumu, alikotafuta usaidizi na kupelekwa kwenye kituo cha kurekebishia tabia kwa muda wa miezi mitatu.

Mkewe, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 48, anaelezea changamoto alizopitia kwa miaka 23 ambayo amekuwa kwenye ndoa.

Maisha ya Bi Florence Wetole yalichukua mkondo mpya, baada yake kukutana na Bw Ochola, wakati huo akiwa bado mwanafunzi.

Hata hivyo, alikuwa bado na uraibu wa pombe.

Ijapokuwa safari yao imejaa changamoto nyingi, inaashiria matumaini na nguvu ya nafasi ya pili anayopata mtu maishani mwake.

Mwanzoni, Bi Wetole, alikuwa na tashwishi wakati Bw Ochola alianza kumweleza kuhusu nia yake kutaka wawe marafiki.

Tashwishi yake ilitokana na uraibu wake wa pombe na mwonekano wake—alikuwa mwembamba sana.

Lakini licha ya changamoto hizo, Florence aliona mwanga katika maisha yake.

“Nilijaribu kumkwepa mara kadhaa, kwani sikuwa tayari kuwa kwenye uhusiano na mlevi. Hata hivyo, hakufa moyo, hadi wakati mmoja nikajiuliza kama nilikuwa na tatizo lolote. Nilijiuliza maswali, kuhusu sababu yangu kuwa kwenye mahusiano na mlevi,” akakumbuka.

Licha ya tashwishi zake, Florence alishindwa kujizuia kukataa rai za Bw Ochola.

Uhusiano wao ulistawi, hali iliyowafanya kuingia kwenye ndoa.

“Sikuogopa, kwani nilipata motisha kutoka kwa mama mkwe,” akasema.

Kwa sasa, Bw Ochola ni mfano bora kuhusu vile mtu anaweza kupata nafasi ya pili maishani.