Makala

Mfumo wa Hydroponic kupunguza gharama ya chakula cha kuku

January 19th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU 

MFUMKO wa bei ya chakula cha mifugo cha madukani ni changamoto kuu kwa wafugaji nchini, ila Joyful Birds Self Help Group ina siri kupunguza gharama. 

Ni kundi la wafugaji 21 wa kuku, lenye makao yake Soweto, mtaani Kayole, Kaunti ya Nairobi.

Aidha, limekumbatia mfumo wa kisasa kuzalisha chakula cha kuku, unaojulikana kama Hydroponic barley fodder.

Barley, kwa Kiswahili ni shayiri na Hydroponic ni teknolojia ya kileo kuzalisha mimea pasi kutumia udongo.

Kulingana na Timothy Malasi, mwanachama wa kundi hilo, wanatumia malighafi yanayopatikana ndani kwa ndani – nchini, na kwa bei ya chini kama kipandio cha shayiri.

Timothy Malasi, memba wa Joyful Birds Self Help Group akielezea kuhusu mfumo wa Hydroponic barley fodder kupunguza gharama ya ufugaji kuku. PICHA|SAMMY WAWERU

“Tunatumia mitungi ya plastiki ya maji, ya lita 20,” Malasi anasema.

Mtungi unagawanywa mara mbili kisha mbegu zinawekwa ndani yake na kunyunyiziwa maji.

Wanachama wa Joyful Birds Self Help Group wanaendeleza ufugaji wa kuku wa mayai walioboreshwa ambao baadaye hugeuzwa kuwa nyama.

Hiyo ikiwa ni biashara inayohitaji mahesabu kupunguza gharama ya malisho, Malasi anasema chini ya siku saba pekee mishayiri huwa tayari kulishwa kuku.

“Kipande kimoja cha mtungi, kinahitaji robo kilo ya mbegu za shayiri. Kiwango hicho, kinapokomaa na kuwa tayari kugeuzwa mlo, kinalisha hadi kuku 20,” alaezea.

Kundi hilo likiwa lilianzishwa 2014, Malasi anaambia Akilimali Dijitali kwamba mbinu hiyo imesaidia wafugaji wanachama kupunguza gharama kwa zaidi ya asilimia 50.

Timothy Malasi akikagua mishayiri ambayo ni tayari kulishwa kuku. PICHA|SAMMY WAWERU

 

Simon Wagura, mtaalamu wa masuala ya ufugaji, anasema shayiri imesheheni karibu asilimia 17 ya virutubisho vya Protini ambayo haijasindikwa (Crude Proteins).

“Hydroponic barley fodder, ni mfumo wa kilimosafi chini ya teknolojia za kisasa kuangazia kero ya mabadiliko ya tabianchi. Wakulima walioukumnatia wanaweza kuendeleza ufugaji hasa wa kuku kuzalisha mazao (mayai na nyama) mfululizo,” Wagura asema.

Licha ya shayiri kuwa na ukwasi wa Protini, mtaalamu huyu anashauri wakulima kusawazisha chakula kiwe na madini mengine faafu kwa kuku kama vile Vitamini, Wanga na Mafuta.

“Kuku, wanahitaji Protini kwa wingi japo ni muhimu pia virutubisho visawazishwe.”

Joyful Birds Self Help Group, ilikuwa miongoni mwa wakulima, kampuni, mashirika na taasisi zilizohudhuria Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Kibiashara Nairobi (ASK) 2023 katika Bustani ya Jamhuri.

Timothy Malasi anasema shayiri ni mojawapo ya malisho ambayo wafugaji wanaweza kukumbatia kupunguza gharama ya chakula. PICHA|SAMMY WAWERU

Shoo hiyo ambayo Malasi alitumia jukwaa lake kuhamasisha wafugaji wa kuku jinsi ya kupunguza gharama ya malisho, ilifanyika kati ya Septemba 25 hadi Oktoba 1.

Tangu 2020, wafugaji nchini wanaendelea kulemewa na gharama ya juu ya chakula cha madukani.

Ongezeko hilo la bei kando na kuchochewa na janga la Covid-20, limezidishwa na kuendelea kupungua na kukosekana kwa malighafi kuunda chakula cha mifugo.

Kenya na ulimwengu, hata hivyo, ilitangaza kuwa huru dhidi ya virusi vya corona.

Mbegu za pamba, halizeti, mahindi na ngano (wheat bran na pollard), ni miongoni mwa malighafi yanayotumika kutengeneza chakula cha mifugo, kile cha kuku kikiandikisha mfumko mkubwa wa bei.

Isitoshe, ushuru wa juu kuagiza bidhaa hizo umechangia hali kuwa mbaya zaidi.

Ndiposa wakulima wanahimizwa, “ikiwa kuna njia au mbinu mbadala hususan ya kujiundia malisho, ni muhimu waikumbatie”.

Mayai ya kuku waliolishwa mishayiri. PICHA|SAMMY WAWERU