Habari Mseto

Mfumo wa kununua ‘token’ uko shwari sasa, KPLC yaambia wateja

June 5th, 2024 1 min read

NA HILARY KIMUYU

KAMPUNI ya umeme nchini (KPLC) imetangaza kuwa imerejesha mfumo wa kununua vifurushi vya stima uliokuwa umesitishwa kwa muda kati ya Juni 2 hadi Juni 3.

Katika taarifa yake Jumanne, kampuni hiyo, ilisema kwamba shughuli ya kutengeneza mfumo wake ilikamilika Jumatatu, mwendo wa saa nne usiku na wateja wanaonunua vifurushi vya stima sasa wanaweza kuvinunua.

“Wateja wetu wanaolipia stima kabla kutumia sasa wanaweza kununua kupitia njia zote ikiwemo Mpesa nambari ya kulipia 888880, Airtel Money na benki. Tunahakikishia Wakenya kwamba tumejitolea kuendelea kuimarisha huduma zetu kukimu mahitaji yao kwa njia bora,” kampuni ilisema.

Shughuli ya ukarabati ilianza saa nne Jumapili usiku na ikachukua muda wa saa ishirini na nne kukamilika na huduma zikarejeshwa saa nne Jumatatu usiku.

Wiki jana, kampuni ilionya kuwa huduma hizo zingetatizika, ikisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuboresha mfumo kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wateja wake.

“Mfumo wa kununua vifurushi vya stima hautapatikana kuanzia saa nne Jumapili usiku Juni 2 hadi saa nne usiku Jumatatu Juni 3, ili kutuwezesha kuboresha mfumo wetu kwa huduma bora zaidi,” kampuni ilisema kwenye ilani wiki jana.