Habari za Kaunti

Mgawanyiko wazuka kuhusu uteuzi wa naibu gavana Uasin Gishu

Na TITUS OMINDE August 24th, 2024 1 min read

MGAWANYIKO umeibuka katika Kaunti ya Uasin Gishu kuhusu uteuzi wa diwani wa Tembilio Evans Kapkea kuchukua nafasi ya Naibu Gavana John Barorot aliyejiuzulu mnamo Agosti 19, 2024.

Baadhi ya wafanyabiashara pamoja na uongozi wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK), wamekosoa uteuzi uliofanywa na Gavana Jonathan Bii.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa CIPK North Rift, Bw Abubakar Bin na Hassan Kosgey, mwanachama mkuu wa jumuiya ya wafanyabiashara mjini Eldoret, viongozi hao walisema hatua ya Gavana Bii haikuzingatia maoni ya viongozi wote katika kaunti.

Walisema uteuzi huo haukuzingatia matakwa ya Gen Z ambao wamekuwa wakilalamika kuwa kaunti imekuwa ikiwatenga katika masuala ya ajira.

Sheikh Bin alisema kwa kuteua diwani ni sawa na kuajiri mtu ambaye tayari anafanya kazi na unampa kazi nyingine.

“Ingekuwa vyema ikiwa gavana angeteua mtu ambaye hajaajiriwa. Tuna vijana wengi waliosoma na walistahili kupewa nafasi ya kuhudumu kwa nafasi hiyo ya naibu gavana,” alisema Sheikh Bin.

Viongozi hao walisema hatua ya kumteua Bw Kapkea itawalazimisha wakaazi wa Tembelio kushiriki uchaguzi mdogo ambao ni ghali na huenda wakasubiri kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC).

Bw Kosgey alisema uteuzi huo unawaweka wakazi wa Tembelio katika njia panda.

“Kuendesha uchaguzi kutakuwa ghali licha ya kuwa hakuna IEBC inayofanya kazi, jambo la busara zaidi ambalo tunatarajia gavana wetu afanye ni kuteua tena mtu mwingine kuchukua nafasi ya naibu wake,” alisema Mzee Kosgei.

Viongozi hao wanawaomba wajumbe wa bunge la Kaunti kutoidhinisha uteuzi huo ili kumruhusu gavana kuteua tena mtu mwingine ambaye hajaajiriwa.

Bw Kapkea ambaye ni diwani wa wadi ya Tembelio vile vile ni mwenyekiti wa Kamati ya Biashara katika bunge la kaunti.

Ana Shahada ya Kwanza katika Kemia ya Uchanganuzi kutoka Chuo Kikuu cha Moi.

Tayari gavana Bii ametuma jina lake kwa bunge la kaunti ili kupigwa msasa.