Habari

Mhadhiri katika chuo kikuu cha MKU ashinda tuzo nyingine

April 19th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MHADHIRI na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya, mjini Thika, Donatus Njoroge, ameshinda tuzo nyingine ya kimataifa kwa ubunifu wa kisayansi na Teknolojia ya GIST,Tech-1.

Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo ya State Department at Global Enterpreneurship ilifanyika katika nchi ya Bahrain mnamo Jumatano, Aprili 17, 2019.

Kulingana na msemaji wa afisi ya mawasiliano kutoka jiji la Washington D.C., Amerika, tuzo hiyo ya Gist Tech- 1 , Pitch, inajumuisha watafiti wengi kutoka nchi tofauti kwa lengo la kuonyesha ujuzi wa ubunifu na utafiti katika nyanja tofauti za kimasomo.

Maswala mengi muhimu yaliyoangaziwa kwa kina ni kuhusu ujuzi wa utafiti, kunoa wale wanaoendesha ubunifu wao na ujuzi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa kwenye ripoti hiyo, washikadau wa kibiashara wapatao 500 waliwasilisha maombi ya ‘Idea Stage’, na 12 ndiyo walifika katika fainali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya, Donatus Njoroge akionyesha tuzo aliyopokea ya GIST Tech-1 ambayo ni ya kimataifa na iliyotolewa nchini Bahrain. Picha/ Hisani

Fedha za kufadhili utafiti zilikuwa ni kati ya Dola 30,000 milioni na dola 200,000 za Kimarekani.

Naibu Chansela katika kitengo cha masomo na utafiti, Dkt Bibianne Waiganjo, alipongeza mhadhiri Njoroge kwa kukiweka chuo Kikuu cha Mount Kenya katika ramani ya Ulimwengu.

“Sisi MKU tunampongeza mmoja wetu kwa kutuangazia sote Ulimwenguni. Utafiti wake wa hapo awali kuhusu maswala ya kuhifadhi chakula ili kisivamiwe na wadudu unaambatana sana na mojawapo ya ajenda kuu nne za serikali. Vile kunatokea ukame kwa sasa  mwenzetu Njoroge atakuwa kama mwalimu wetu kuhusu uhifadhi wa chakula,” alisema Dkt Waiganjo.

Katika kiwango cha ‘Start Up’  baadhi ya washindi  kwa utafiti na ubunifu walikuwa, Donatu Njoroge, (Vinis  Limited), Kenya.

Wa pili ni Abraar Ahmed Azard, (Health private Limited), Pakistan.

Wa tatu ni Varinder Singh (GFF Innovation Pvt Ltd) India.

Wengine waliotuzwa kutoka nchi tofauti kiwango cha ‘ Idea Phase’ ni Anatoli Kirigwajjo (Yunga Technologies), Uganda.

Pia Isaac Sesi, (Sesi Technologies Ltd) wa Ghana, na Aviuntuya Altangerel, (Brighton English Speaking Centre), Mongolia.

Tangu kuzinduliwa kwa mashindano hayo ya GIST, 2011,  yamejumuisha washikadau au wanachama kutoka ulimwenguni kote wapatao 27 milioni, huku wasomi wapatao 137 kutoka nchi wanachama wakiwa wamenolewa kwa maswala ya utafiti.

Wameweza kupokea ushuru wa Dola 250 milioni, na kubuni ajira kwa watu wapatao 6,000 hadi kufikia mwaka 2018.

Kulingana na ripoti hiyo jamii ya shirika la GIST, imenufaika kutokana na kiwango cha takribani Dola 1,000,000 kupitia tovuti ya Amazon Web Services, Microsoft, Google na sekta za kibinafsi.