Makala

Mhubiri anayelisha waumini wake chakula cha kiroho na cha kimwili vile vile kupitia kilimo

February 20th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

HATA ingawa kijiji cha Kamale, Kitui Mashariki hakikosi kuhangaishwa na kiangazi, kina sifa za kipekee kufuatia jitihada za mchungaji anayejituma kukibadilisha kiwe Israili ndogo.

Sawa na maeneo mengine katika Kaunti ya Kitui, ndengu, mahindi na maharagwe yanakuzwa kwa wingi ila katika mgunda wa David Mutinda taswira ni tofauti.

Mutinda ni mhubiri wa Kanisa la Deliverance tawi la Kitui Mashariki ambaye kando na kulisha washirika wake chakula cha kiroho anawahamasisha kuhusu kilimo bora.

Ni katika mukhtadha huo, anawafumbua macho kuhusu ulaji wa vyakula vyenye virutubisho.

“Kati ya aina 10 ya mseto wa vyakula vinavyoshabikiwa, aghalabu binadamu anapaswa kula aina isiyopungua 5 kwa siku ili kuafikia vigezo vya lishe bora,” Mutinda anasema.

Kwenye shamba lake, ana bustani yenye mseto wa mimea, hususan, mboga.

Mchungaji David Mutinda shambani mwake Kaunti ya Kitui akiondoa kwekwe kwenye mboga. PICHA|SAMMY WAWERU

Awali, mkulima huyu anasema watoto eneo analoishi walikuwa wenyeji hospitalini kwa sababu ya maradhi ya utapiamlo.

Hata hivyo, tangu mwaka 2020, janga la Covid-19 lilipotua nchini (japo ulimwengu ulitangazwa kuwa huru dhidi ya virusi hatari vya corona miaka mitatu baadaye), alipoanzisha bustani ya mimea inayochukua muda mfupi kukomaa, Mutinda anakiri visa vya watoto kuugua maradhi yanayohusishwa na ukosefu wa virutubisho vya kutosha mwilini vimepungua.

Kwenye bustani yake, ameipamba kwa mboga za kienyeji, kuanzia mnavu (maarufu kama sucha au managu), mchicha (terere), kunde, sukuma wiki, spinachi na kabichi.

Hali kadhalika, anakuza viungo vya mapishi kama vile nyanya, pilipili mboga (almaarufu hoho), vitunguu, dhania na biringanya.

Isitoshe, analima matunda kama vile maembe na ndizi.

Pasta Mutinda anatumia jukwaa hilo kupevusha wenyeji kuhusu lishe bora, akihudumu kwenye kikundi chenye wanachama 150 anaongoza.

“Tangu niingilie kilimo cha mseto wa mimea inayochukua muda mfupi kukomaa, nimeweza kufikia zaidi ya wakulima 500 na kuwahamasisha jinsi wanavyoweza kuvuna maji na kugeuza mashamba yao kuwa mabustani,” anaelezea.

Ana kisima cha maji chenye kina cha urefu wa futi 50 na anatumia kawi ya jua (sola) kuvuta maji na kuyasambaza, mfumo wa kisasa kuendeleza zaraa anaosema alipigwa jeki na United States Agency for International Development (USAID) kupitia Shirika la Agricultural Development Services (ADS) eneo la Mashariki mwa Kenya, 2022.

David Mutinda ana kisima cha maji. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, ana sola yenye Mega Wati 1, 500.

“Kupitia ADS, nilipokea mafunzo ya kilimo endelevu na jinsi ya kuangazia lishe bora,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano shambani mwake Kijiji cha Kamale.

Mbali na kuwafaa wakulima, Mutinda alisema hulisha familia yake kupitia mradi huo na pia hufanya mauzo ya mazao mabichi.

“Kwa siku, nikiwa na mavuno sikosi kuingiza Sh1, 000,” alisema.

Mifumo, teknolojia na bunifu za kisasa kuendeleza kilimo ni kati ya mbinu ambazo zinahamasishwa na wataalamu na wadau katika sekta ya kilimo.

“Endapo kuna mbinu ambazo zitasaidia kuangazia kero ya njaa na uhaba wa chakula nchini, ni ukumbatiaji wa teknolojia na kuendeleza kilimo cha kisasa (smart agriculture technologies and solutions),” katibu katika Wizara ya Kilimo, Dkt Paul Ronoh, akaambia Akilimali hapo awali kupitia mahojiano ya kipekee.

Mifumo ya kisasa inajumuisha uvunaji maji, matumizi ya mashine na mitambo, unyunyiziaji mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji (irrigation), upanzi wa mbegu zilizoboreshwa kustahimili makali ya kiangazi na ukame, kati ya mingineyo.

Mhubiri David Mutinda, anasema ni kwa muda tu ageuze shamba lake kuwa uga wa kumezewa mate na hata kutoa mafunzo ya kilimo bora na endelevu Kaunti ya Kitui.