Michezo

Aduda alia mashabiki hawafiki uwanjani

February 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

USIMAMIZI wa Mabingwa mara 17 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) Gor Mahia umesikitikia idadi ndogo ya mashabiki wanaojitokeza kushabikia timu hiyo katika mechi za kuwania kufuzu robo fainali ya Kombe la Mashirikisho Barani Afrika (CAF).

Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda amesema hali hiyo imechangia wachezaji kutokuwa na motisha huku akiwarai wafike kwa wingi katika uwanja wa MISC Kasarani kesho kutwa kushabikia timu yao.

K’Ogalo Jumapili hii watatifua vumbi dhidi ya Hussein Dey ya Algeria kwenye mechi ya Kundi D ya mashindano hayo.

“Tunasikitishwa sana na idadi ya mashabiki wanaohudhuria mechi zetu za CAF katika. Wachezaji wetu huingiwa na kiwewe wanaposhiriki mechi za ugenini uwanja wa wenyeji wao ukiwa umefurika furi furi ilhali kwao nyumbani mashabiki wakuhesabika tu ndio hujitokeza,” akasema Aduda kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

“Tunaposhindwa ni mashabiki wawa hawa wanaopiga kelele kwa sauti ya juu wakipendekeza mabadiliko ilhali siku za mechi hawapatikani kuwapa wachezaji motisha na kuchangia ushindi,” akaongeza.

Hata hivyo alisema kama ofisi, wanapanga kuwasilisha maoni ya mashabiki kwa kocha Hassan Oktay kuhusu idara ya unyakaji baada ya wengi wao kulalamikia kuhusu kushuka kwa mchezo wa nyani Boniface Oluoch wakitaka kipa nambari mbili Peter Odhiambo kupangwa katika kikosi cha kwanza.

“Vilio, maoni na mapendekezo yote ya mashabiki yatawasilishwa kwa kocha ili aweze kufanya marekebisho haswa kuhusu nafasi ya mlinda lango ambayo inaendelea kuzua malalamishi. Hata hivyo hatutamshinikiza ama kumlazimisha kwasababu uamuzi wa nani kupangwa kikosini ni wake,” akasisitiza.

Ingawa hivyo, aliwataka mashabiki kusheherekea mabao ya timu hiyo kwa ustaarabu badala kurusha chupa na mawe uwanjani jinsi ilivyokuwa wakati wa mechi dhidi ya Zamalek kutoka Misri kuwaepushia adhabu ya CAF.

Hussein Dey wanaongoza kundi D, waliwasili nchini jana ili kujifua kabla ya ngarambe hiyo muhimu kwa K’Ogalo wanaoshikilia nafasi ya tatu.

Jacques Tuyisenge, Boniface Omondi, Samuel Onyango na Dennis Oliech wanatarajiwa kuongoza uwindaji mabao kwa K’Ogalo siku ya Jumapili.