Michezo

AFC Leopards SC yaipiga Western Stima 2-1

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MARCEL Kaheza amekuwa shujaa wa AFC Leopards SC baada ya kuifungia bao la ushindi ikibwaga Western Stima 2-1 kwenye Ligi Kuu Jumamosi uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Mvamizi huyu kutoka Tanzania, ambaye alijiunga na Leopards katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichopita kutokea Simba SC, liingia uwanjani kama mchezaji wa akiba dakika ya 52.

Alichukua nafasi ya Brian Marita, ambaye alikuwa amepoteza nafasi kadhaa nzuri katika kipindi cha kwanza.

Dakika 90 zilitamatika 1-1 Vincent Oburu akiwa amesawazishia Ingwe dakika ya 52 baada ya Wesley Kemboi kuweka wanaumeme wa Stima mbele dakika ya 36.

Hata hivyo, Kaheza alihakikishia waajiri wake ushindi alipojaza wavuni bao la ushindi sekunde chache baada ya muda wa majeruhi kukatika dakika ya 94.

Baada ya kuzoa ushindi dhidi ya Stima kwa mara ya kwanza katika mechi nne, mabingwa mara 13 Leopards sasa wameruka Vihiga United, Chemelil Sugar, Posta Rangers na Zoo na kuzisukuma chini nafasi moja kila mmoja hadi nambari 14, 15, 16 na 17, mtawalia.

Ingwe ni ya 13 kwa alama 19.

Iliingia mechi ya Stima ikishikilia nafasi ya 17, moja kutoka mkiani. Stima, ambayo haijashinda katika mechi sita zilizopita, inashikilia nafasi ya tisa kwa alama 23.

Timu za Stima na Ingwe zitarejea uwanjani Machi 27 kukabana koo na 12 nambari KCB na Vihiga, mtawalia.

Katika mechi nyingine iliyochezwa Jumamosi, Chemelil Sugar imeendeleza ukame wa Bandari kutoshinda mechi hadi mechi nne baada ya kuilazimishia sare tasa mjini Chemelil.

Nambari mbili Bandari imezoa alama 33. Iko nyuma ya viongozi Sofapaka kwa tofauti ya magoli.

Chemelil ni nambari 15 kwa alama 18. Bandari itaalika nambari nane Kakamega Homeboyz katika mechi yake ijayo Machi 27 nayo Chemelil itakuwa mwenyeji wa nambari saba Tusker siku hiyo.

Mechi moja itasakatwa Jumapili ambapo Posta Rangers itaalika KCB.

Rangers haina ushindi katika mechi tatu zilizopita. KCB ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nzoia 2-0 katika mechi yake iliyopita mnamo Machi 10.