AFCON 2019: Zifa yatangaza kikosi cha Zimbabwe licha ya wachezaji kutishia kugoma
Na GEOFFREY ANENE
SAA chache kabla ya Kombe la Afrika (AFCON) kung’oa nanga nchini Misri hapo Juni 21, masuala ya migomo ya wachezaji imejitokeza katika kambi ya Zimbabwe.
Taarfa kutoka nchini Zimbabwe zinasema kwamba wachezaji wametisha kususia mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Misri itakayosakatwa saa tano usiku Ijumaa jijini Cairo.
Wachezaji na maafisa wa timu hiyo almaarufu kama Warriors, ambao hawakutaka kutajwa, wamenukuliwa na vyombo vya habari nchini Misri wamefanya mkutano na viongozi wa Shirikisho la Soka la Zimbabwe (ZIFA), lakini suluhu haikupatikana.
“Wachezaji walikataa kufanya mazoezi na wanataka kulipwa marupurupu yao pamoja na ada ya kuwa timuni katika mashindano walioshiriki mwezi Mei,” habari zinasema, huku mchezaji mmoja akisema kuna wachezaji waliotaka waruhusiwe kutoka kambini waende nyumbani.
Inasemekana kwamba ZIFA ilikuwa imepuuzilia habari hizo, lakini wachezaji watano na afisa mmoja walitembelea vyombo vya habari.
Hata hivyo, tunavyzungumza, ZIFA, kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter, imetaja kikosi kitakachoanza mechi dhidi ya Misri.
Tendai Darikwa, Divine Lunga, Alec Mudimu, Teenage Hadebe, Marshall Munetsi, Marvelous Nakamba, Ovidy Karuru, Knowledge Musona, Khama Billiat na Nyasa Mushekwi wako katika kikosi cha wachezaji 11 cha kocha Sunday Chidzambwa.