AIBU KUU: Origi abaguliwa kwao nchini Ubelgiji
Na MASHIRIKA
GENK, UBELGIJI
LIVERPOOL imeshutumu vikali bango la kumbagua Divock Origi kwa sababu ya rangi yake lililowekwa katika eneo la mashabiki wa timu hiyo ya Uingereza kabla ya mechi dhidi ya Genk nchini Ubelgiji mnamo Jumatano.
Bango hilo lilionekana kuonyesha kichwa cha Origi kilichotundikwa juu ya mwili uliokuwa uchi kando ya kombe la Klabu Bingwa Ulaya.
Liliondolewa kabla ya mechi hiyo kuanza.
Taarifa kutoka kwa klabu ilisema, “Klabu ya soka ya Liverpool inalaani bango la kukera lililowekwa katika sehemu ya mashabiki wetu kabla ya mechi kuanza.
“Bila shaka, picha hiyo ilitumiwa kueneza ubaguzi wa rangi. Hiki ni kitendo kisichokubalika kabisa.
“Tulihakikisha bango hilo linaondolewa haraka iwezekanavyo na sasa tunashirikiana na viongozi wa eneo hili pamoja na wasimamizi wa uwanja wa mjini Genk kutambua wale waliohusika.
“Hatua yoyote itachukuliwa kuhakikisha wahusika wanaadhibiwa.”
Alipoulizwa kuhusu maoni yake baada ya mechi, kocha Jurgen Klopp alijibu, “Sikuona bango hilo, lakini nilisikia kuwa tayari tumeshatoa taarifa kwa hivyo sina la kuongeza.”
Liverpool ilishinda mchuano huo kwa mabao 4-1. Origi aliijaza nafasi ya Roberto Firmino baada ya Mbrazil huyo kupumzishwa katika dakika ya 80.
Origi, ambaye wazazi wake ni Wakenya, alizaliwa mjini Ostend nchini Ubelgiji miaka 24 iliyopita. Talanta yake ya uchezaji ilikuzwa katika akademia ya Genk.
Hapo Jumatano, alikaribishwa uwanjani Luminus Arena kwa shangwe alipoingia kama mchezaji wa akiba na pia baada ya mechi kutamatika.
Mabao mawili
Aidha, Klopp alikiri kufurahishwa na Alex Oxlade-Chamberlain baada ya kiungo huyu kutumia fursa ya kuanzishwa kwenye mechi kupachika mabao mawili muhimu.
Mwingereza huyu, ambaye alikosa kipindi kikubwa cha msimu uliopita akiuguza jeraha na amekuwa akitumiwa mara moja moja msimu huu, alifungua akaunti ya magoli dakika ya pili uwanjani Luminus Arena.
Kisha, aliimarisha uongozi huo hadi 2-0 kwa kukamilisha shambulio kwa ustadi kutoka nje ya kisanduku dakika ya 57.
Sadio Mane aliongeza bao la tatu dakika ya 77 kabla ya Mohamed Salah kuhitimisha mabao ya Liverpool dakika 10 baadaye. Stephen Odey, ambaye aliingia nafasi ya Paul Onuachu dakika ya 81, alifungia Genk bao la kufutia machozi dakika ya 88.
“Alikuwa na kipindi kizuri kabisa uwanjani. Mchezo wa Ox ulikuwa sawa kabisa na ule wa timu – mabao yalikuwa ya kusisimua, ingawa hata hao wengine wangefanya bora, lakini hivyo ndivyo mambo huwa, hakuna tatizo,” alisema Klopp.
Mchango wa Ox ulikuja siku chache baada ya mchezaji mwingine asiyetumiwa sana, Adam Lallana, kutikisa nyavu za Manchester United katika dakika za lala-salama timu hiyo ikitoka sare ya 1-1 wikendi iliyopita.
“Mabao hayo yalikuwa ya kipekee na muhimu sana kwetu – ilifurahisha sana Jumapili wakati Adam alipachika bao hilo na sasa, Ox amefunga mabao mawili.”
Oxlade-Chamberlain, 26, alirejea kutoka mkekani baada ya kupona jeraha baya la goti kabla tu ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita.