Aisee, hivi hawa Manchester United wameamka kabisa kabisa au ni moto wa karatasi tu?
MANCHESTER UNITED wanaonekana kuamka baada ya kuagana na Erik ten Hag na kumpa majukumu naibu wake Ruud van Nistelrooy kama kaimu kocha baada ya ushindi mkubwa wa 5-2 dhidi ya wapinzani wenzao kutoka Ligi Kuu, Leicester kwenye kipute cha Carabao ugani Old Trafford, Jumatano.
Ushindi huo wa kwanza katika mechi tatu zilizopita na wa pili katika mechi tisa msimu huu ulipatikana kupitia mabao ya Casemiro (dakika ya 15 na 39), Alejandro Garnacho (28) na Bruno Fernandes (36 na 59). Foxes walijiliwaza na magoli kutoka kwa Bilal El Khannouss (33) na Conor Coady (45+3).
Ni mara ya kwanza United kushinda Leicester kwa mabao matano au zaidi tangu ushindi wa 6-2 mnamo Januari 1, 1999.
Rekodi ya kukalafisha Leicester City
United sasa wamepepeta Leicester mara tatu mfululizo kwa jumla ya mabao 9-3. Hata hivyo, swali linalosalia ni je, United wameamka kabisa ama ni moto wa karatasi? Muda ndio utakuwa msema kweli kuanzia Jumapili watakapoalika Chelsea ugani Old Trafford kwa majukumu ya ligi.
Katika jedwali la ligi ya EPL, Chelsea waliopoteza 2-0 dhidi ya Newcastle katika Carabao hapo Jumatano, wapo nafasi ya tano kwa alama 17. Mashetani wekundu United wanaonyemelea kocha wa Sporting Lisbon, Ruben Amorim, wako nafasi ya 14 kwa alama 11 baada ya kupoteza mechi ya nne kwa kuduwazwa na West Ham 2-1 Oktoba 27.