Ajabu ya Misri kufuzu kwa alama tatu bila ushindi katika mechi tatu AFCON
NA LABAAN SHABAAN
MISRI ilinyemelea na kupenya hadi mkondo 16 wa Dimba la Kandanda la Afrika 2023 (AFCON) katika usiku wa drama walipolimana na Cape Verde.
Zilihitajika mechi tatu za sare ya mabao mawili kwa Egypt kushusha pumzi tayari kwa pambano la awamu ya kuondoana.
Kipute hiki kiliisha na sare ya 2 – 2 baada ya Cape Verde kufunga bao dakika ya lala salama.
Mechi ilitamatika huku Mafarao wakidhani wamebanduliwa Cape Verde iliposawazisha dakika ya 99.
Wachezaji wa Misri walionekana wanyonge kwa sawazisho hilo na nyuso zao zilisawijika matumaini yao yakisambaratika.
Hawakujua wamefuzu kwa kupata sare hii huku Ghana ikipokonywa tonge mdomoni na Msumbiji kipindi cha lala kwenye mkono wa buriani.
Soma Afcon: Mataifa yaliyodunishwa yahangaisha mibabe
Pia KBC yakemewa kwa upeperushaji mbovu wa Afcon
Wakati huo, mechi sambamba ya kundi B ilikuwa nusura iishe 2 – 1 kati ya Msumbiji na Ghana.
Hii ilikuwa kwa faida ya Ghana lakini Mozambique ikasawazisha dakika ya 94.
Matokeo haya yalisaidia Misri kufuzu wakiwa namba mbili nyuma ya Cape Verde walioibuka kidedea kwa alama 7.
Ghana na Msumbiji walioambulia pointi mbili na moja mtawalia walionyeshwa mlango wakaaga mashindano.
Misri iliyokosa huduma za nyota wao Mshambulizi stadi wa Liverpool ya Uingereza – Mohamed Salah – ilianza pambano dhidi ya Cape Verde kwa kufungwa bao na Gilson Tavares dakika ya 46 kabla ya wao kusawazisha dakika nne baadaye kupitia Mshambulizi Mahmoud Ahmed maarufu Trezeguet.
Naye Mostafa Mohamed aliweka Misri kifua mbele dakika ya majeruhi ya 93 alipopokea mkwaju mrefu na murua kutoka kwa Trezeguet.
Cape Verde walizidi kubisha lango la Misri na wakafunguliwa dakika ya 99 baada ya Bryan Teixeira kumzunguka kipa na kutikisa wavu.
Mafarao wamezidi kuwa na moyo mgumu na sasa wako katika mkondo wa 16 wakisaka taji lao la 8 la kombe la AFCON.
Ndilo taifa lililoshinda kombe hili mara nyingi zaidi kushinda mataifa mengine Afrika.
Mchanganuzi wa Kandanda na Mwanahabari Peter Pinchez Mwaura anakiri imekuwa kama miujiza kwa Misri kutinga orodha ya 16 bora ila anadokeza timu hii itabadilisha mbinu katika hatua hiyo.
“Misri sasa wanaonekana kama wako gizani lakini wanaweza kuwashangaza wengi wakionekana kwenye fainali,” akasema Bw Mwaura ambaye anahisi kutoonekana kwa Mo Salah kutasaidia timu pinzani ziwaone kama wanyonge na hali aghalabu hawategemei wachezaji nyota kupata matokeo mazuri.
Iliyosomwa sana Wakenya kutazama Tanzania ikihangaika huko AFCON kupitia KBC bila malipo