Allegri aapa kuikung'uta Altetico ikizuru Turin
NA CECIL ODONGO
MADRID, UHISPANIA
MKUFUNZI Mkuu wa timu ya Juventus, Massimiliano Allegri amesema kwamba ana wingu la matumaini la kukomboa mabao mawili waliyofungwa na Atletico Madrid kwenye mechi ya Klabu Bingwa Barani Uropa(UEFA) Jumatano Februari 20, 2019.
Allegri amesema kwamba timu yake itajituma vilivyo katika mkondo wa pili wa mtanange huo unaotarajiwa kusakatwa katika jiji la Turin, Italia mwezi ujao wa Machi.
Kikosi cha Diego Simeone kilionyesha mchezo wa juu na kubamiza mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu nchini Italia (SERIE A) huku nyota wao Juve Cristiano Ronaldo akionyesha mchezo duni na kusababisha kufungwa kwa bao la pili.
Kichapo hicho kilirejesha kumbukumbu ya mwaka wa 2018, Juve ilipochapwa nyumbani 3-0 na mabingwa watetezi wa kipute hicho Real Madrid lakini nusura wageuze kichapo hicho uwanjani Santiago Bernabeu walipotandika wapinzani wao 2-0 kwenye mechi ya mkondo wa pili.
“Hutukufifishwa matumaini na kichapo cha 3-0 mikononi mwa Real Madrid mjini Turin msimu wa 2018 na hali inasalia vivyo hivyo msimu huu. Lazima tukisahau kichapo hiki haraka iwezekanavyo na tucheze vizuri nyumbani ili kufutilia mbali ushindi wao,” akasema Allegri.
Mkufunzi huyo wa zamani wa AC Milan aliwataka wachezaji wake kutoangazia sana matokea hayo na badala yake wavumbue mbinu wakatakazotumia kuiliza Atletico kwenye mechi ya mkondo wa pili ili waweze kufuzu hatua ya robo fainali ya ligi hiyo ya uchampioni.
“Ni vizuri kabla ya mechi hiyo, wachezaji wetu wanaouguza majeraha watakuwa wamerejea kikosini. Najua halitakuwa jambo rahisi kukigeuza kichapo hiki jijini Turin lakini hakuna lisilowezekana,” akasisitiza Allegri.