Michezo

Alvaro Morata arudi Juventus kwa mkopo kutoka Atletico Madrid

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

JUVENTUS wamemsajili upya mshambuliaji Alvaro Morata, 27, kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Atletico Madrid.

Raia huyo wa Uhispania atavalia sasa jezi za Juventus ambao ni miamba wa soka ya Italia hadi mwishoni mwa msimu wa 2020-21 na kikosi hicho cha kocha Andrea Pirlo kitakuwa radhi kurefusha kandarasi ya Morata kwa miezi 12 zaidi au kumpa mkataba wa kudumu kabisa kwa bei itakayopendekezwa na Atletico.

Kwa sasa, Juventus watawalipa Atletico kiasi cha Sh1.3 bilioni kwa kila msimu ambao watajivunia huduma za Morata kwa mkopo.

Alitia saini mkataba wa kudumu kambini mwa Atletico mnamo Julai 1, 2020, baada ya kuwachezea kwa kipindi kirefu kwa mkopo kutoka Juventus.

Atletico wametaka Juventus kuweka mezani Sh5.7 bilioni iwapo watataka kumsajili Morata kwa mkataba wa kudumu mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21 au Sh4.5 bilioni iwapo wataamua kumtwaa kabisa mwishoni mwa wa 2021-22.

Morata aliwahi kucheza Juventus kati ya 2014 na 2016 na akawasaidia kunyanyua mataji mawili ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Tangu wakati huo amechezea Real Madrid na Chelsea kwa mikataba ya kudumu kabla ya kujiunga na Atletico kwa mkopo wa miezi 18.

Juventus wanalenga kutia kibindoni taji la Serie A kwa mara ya 10 mfululizo msimu huu na walianza kampeni za kuhifadhi ufalme wa kipute hicho kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Sampdoria mnamo Septemba 20, 2020.