Michezo

AMHITAJI WENGER: Ljungberg kushauriwa kabla ya Arsenal kualika Brighton

December 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA wa muda, Freddie Ljungberg anapanga kushauriwa na mkongwe Arsene Wenger kabla ya Arsenal kucheza na Brighton leo Alhamisi usiku, ugani Eimrates.

Raia huyo wa Uswidi alishuhudia kama shabiki vijana hao wakitoka sare 2-2 na Norwich mnamo Jumapili, lakini amesema atashauriana na Wenger kabla ya kuanza kazi rasmi leo Alhamisi.

Arsenal wamecheza mechi nane bila kushinda chini ya Unai Emery aliyetimuliwa majuzi baada ya mashabiki kulalamika vikali.

“Ningependa kuzungumza na Wenger kabla ya kucheza na Brighton,” alisema kiungo huyo wa zamani ambaye alisajiliwa na Wenger mnamo 1998 akitokea Halmstad. Naendelea kumtafuta kwa simu lakini sijampata. Alikuwa hapa miaka 22 kama kocha, hivyo ana ujuzi mwingi. Na huenda kuna mambo fulani ambayo angependa yafanyike ili kazi yangu iwe rahisi. Lazima nimpate.”

Tayari Wenger aliahidi kumsaidia Ljungberg katika juhudi za kutekeleza wajibu wake pale Emirates. Roho yangu ingali kwa Arsenal. Na ningependa wacheze vizuri chini ya Freddie. Tungependa kumsaidia afaulu katika kazi yake.”

Mbali na Wenger, kadhalika Ljungberg amepata ushauri kutoka kwa kocha mkongwe wa kimataifa Sven-Goran Eriksson, raia wa Sweden.

“Sven ni mwerevu sana. Nimezungumza naye mara kwa mara kwa sababu alipokuwa kocha wa timu ya Uingereza alihudhuria mechi zetu kadhaa. Nakumbuka alivyowafanya wachezaji wafurahie. Nimeiga baadhi ya mbinu zake, na nitaendelea kuzungumza naye.”

Arsenal wanatafuta kocha wa kudumu baada ya kuagana na Emery, na huenda Brendan Rodgers wa Leicester City akapewa nafasi hiyo mwishoni mwa msimu huu.

Kuhusu usajili

Tayari Ljungberg amesema hafikirii kufanya usajili wowote wa nguvu wakati wa shughuli za wachezaji kubadilisha timu, ingawa matokeo ya timu hairidhirishi.

Kwa sasa mashabiki wa Arsenal wanatafakari kwa mfumo watakaoucheza chini ya Rodgers ambaye anatarajiwa kuanza kuinoa klabu hiyo kama kocha wa kudumu.

Baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Everton kocha huyo alijibu swali la kuhusishwa na Arsenal ambayo majuzi ilimtimua Emery.

Rogers alisema mkataba wake na Leicester City unamruhusu kuondoka iwapo atapata ofa nyingine.

Rodgers yuko katika orodha ya makocha wanaohusishwa kujaza nafasi ya Emery pamoja na Mauricio Pochettino aliyetimuliwa na Tottenham Hotspur.

“Kwa sasa siwezi kusema lolote, labda niwahakikishie kwamba mkataba wangu upo wazi, naweza kuondoka kama nitapata dili nyingine, lakini sio rahisi kupata dili kama mnavyofikiria,” aliongeza.

“Ligi imefikia hatua ngumu kwa sasa na ningependa nielekeze mawazo yangu kwa timu ili imalize katika nafasi nzuri,’ alisema kocha huyo wa zamani wa klabu ya Celtic ya Scotland.

Arsenal inakamata nafasi ya nane jedwalini baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 19.