Michezo

Ancelotti adai ataiondoa Arsenal Europa

April 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI Mkuu wa Napoli FC Carlo Ancelotti ameiambia Arsenal kusahau uwezo wowote wa kupiga hatua kwenye kipute cha robo fainali ya Kombe la Ligi ya Uropa, siku 10 tu kabla timu hizo kukutana ugani Emirates April 11.

Ingawa alikiri kwamba Arsenal itatoa upinzani mkali kwa Napoli inayoendelea kutesa sana katika Ligi ya Serie A, Ancelotti amesema liwalo na liwe lazima waibandue Arsenal kwa kushinda mechi ya mkondo wa kwanza kisha kuhitimisha kazi wakati wa mechi ya mkondo wa pili.

“Najivunia usemi na utabiri wa wengi wanaotupigia upato wa kutwaa Ligi ya Uropa. Hata hivyo tuna mechi kali ya robo fainali dhidi ya Arsenal ambayo lazima tuishinde Aprili 11 katika uwanja wao wa nyumbani. Ingawa haitakuwa mechi rahisi, tuna matumaini makubwa ya kuwabagwa na kutinga nusu fainali,” akasema Ancelotti ambaye aliwahi kufundisha soka klabu za Chelsea, AC Milan na Real Madrid.

Nafuu kwa Napoli hata hivyo ni kwamba baadhi ya wachezaji wa tegemeo watakuwa wanarejea baada ya kipindi kirefu cha majeraha. Mshambulizi matata Lorenzo Isigne atakuwa kati ya wachezaji hao na anatarajiwa kuongoza safu hiyo kutatiza difensi ya Arsenal ambayo imekuwa ikivuja sana katika mechi za EPL.

Napoli wamekuwa na fomu ya kutisha kwenye Serie A baada ya kuinyeshea mvua ya mabao AS Roma 4-1 Jumapili Machi 31, matokeo yaliyojiri siku chache walipozidia nguvu Udinese kwa kuisakama 4-2.