Michezo

Argentina wawafagia Qatar, sasa ni Venezuela robo fainali

June 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

PORTO ALEGRE, BRAZIL

NYOTA wa Manchester City, Sergio Aguero aliwafungia Argentina bao la pili katika ushindi wa 2-0 waliousajili dhidi ya Qatar kwenye mojawapo ya mechi za kuwania ubingwa wa taji la Copa America mnamo Jumapili usiku, japo katika awamu ya makundi.

Mabingwa hawa wa 1991 na 1993 kwa sasa watavaana na Venezuela katika robo-fainali itakayowakutanisha katika uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro, Brazil mnamo Juni 28.

Venezuela walitinga hatua ya nane-bora katika kipute cha mwaka huu baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye Kundi A lililotawaliwa na wenyeji Brazil kwa alama saba.

Peru walikamilisha kampeni zao za Kundi A katika nafasi ya tatu kwa alama nne huku Bolivia wakiaga mapema michuano hiyo baada ya kushindwa kuzoa alama yoyote kutokana na mechi tatu.

Aguero alivurumisha kombora kutoka hatua ya mita 13 na kutikisa nyavu za Qatar ambao walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara.

Awali, kiungo Lautaro Martinez ambaye kwa sasa huchezea kikosi cha Inter Milan nchini Italia alikuwa amewafungia Argentina bao la ufunguzi katika dakika ya nne ya kipindi cha kwanza.

Bao la Martinez lilikuwa zao la mvamizi Bassam Al-Rawi wa Qatar ambaye alishuhudia fataki yake kunako dakika ya 86 ikibusu mwamba wa goli la Argentina.

Matokeo hayo yalitosha kuwabandua Qatar kwenye fainali za Copa America. Japan na Qatar waliokuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022 walikuwa waalikwa katika fainali za Copa America zilizoleta pamoja mataifa yote 10 ya Amerika Kusini mwaka huu.

Argentina waliambulia nafasi ya pili nyuma ya Colombia ambao walidhibiti kilele cha Kundi B baada ya kujizolea jumla ya alama tisa.

Licha ya kujivunia huduma za nahodha na mvamizi matata wa Barcelona Lionel Messi, Argentina walitia kapuni alama nne pekee, mbili zaidi kuliko Paraguay ambao walizamishwa 1-0 na Colombia katika mchuano mwingine wa Jumapili.

Chini ya kocha Lionel Scaloni, Argentina ambao ni mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia, kwa sasa wanapigiwa upatu wa kutwaa ufalme wa Copa America mwaka huu baada ya kuzidiwa maarifa na Chile katika makala mawili yaliyopita mnamo 2015 na 2017.

Hata hivyo, huenda kibarua kilichopo mbele ya Argentina kikawa kigumu hata zaidi hasa baada ya kutowaridhisha mashabiki walipokuwa wakichuana na Qatar ambao wanashikilia nafasi ya 55 duniani kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Ushindi wa lazima

Mchuano dhidi ya Qatar ulikuwa wa lazima kwa Argentina kusajili ushindi hasa baada ya kufungua kampeni za Kundi B kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Colombia Juni 16 kabla ya Paraguay kuwalazimishia sare ya 1-1.

Kichapo cha 1-0 ambacho Colombia waliwapokeza Paraguay katika mechi ya mwisho ya Kundi B pia kilichangia pakubwa kusonga mbele kwa Argentina.

Vikosi vingine ambavyo tayari vimetinga robo-fainali za Copa America mwaka 2019 ni Chile, Colombia na Brazil ambao waliwakomoa Peru 5-0 mwishoni mwa wikendi iliyopita.

Jumatatu ilikuwa zamu ya mabingwa watetezi Chile kupimana ubabe na Uruguay ambao wanajivunia huduma za wavamizi Luis Suarez na Edinson Cavani wa Barcelona na PSG mtawalia. Katika mechi nyingine ya Kundi C, Ecuador walipepetana na Japan.