• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Argentina ya Messi hatarini kuaga Copa America

Argentina ya Messi hatarini kuaga Copa America

Na MASHIRIKA

PORTO ALLEGRE, Brazil

WAFALME wa Copa America mwaka wa 1991 na 1993 Argentina wanakabiliwa na hatari ya kuaga makala ya mwaka 2019 yanayoendelea nchini Brazil.

Argentina, ambayo inajivunia kuwa na sogora bingwa mara tano wa tuzo ya mwanasoka bora duniani Lionel Messi inavuta mkia katika Kundi B linalojumuisha Colombia, Paraguay na Qatar.

Colombia inaongoza kundi hili kwa alama sita baada ya kubwaga Argentian 2-0 kupitia mabao ya Roger Martinez na Duvan Zapata na kupepeta Qatar 1-0 kupitia bao la Zapata.

Paraguay ni ya pili kwa alama mbili baada ya kutoka 2-2 dhidi ya wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022 Qatar na kuandikisha 1-1 dhidi ya Argentina.

Penalti ya Messi katika kipindi cha pili dhidi ya Paraguay ilisaidia Argentina kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.

Hata hivyo, ili kufika robo-fainali kwenye mashindano haya ya mataifa 12, sharti Argentina lipige Qatar mjini Porto Allegre, leo.

Argentina itabanduliwa nje ya mashindano haya iwapo itapokea kichapo ama sare dhidi ya Qatar.

Argentina itaanza mechi dhidi ya Qatar na rekodi nzuri baada ya kucharaza mabingwa hao wa Bara Asia mabao 3-0 katika mechi moja ambayo walikutana mwaka 2005 katika mechi ya kirafiki.

Habari nzuri zaidi katika kambi ya Argentina ni kwamba Qatar haijawahi kupata ushindi dhidi ya mpinzani kutoka Amerika Kusini.

Waarabu

Waarabu hao, ambao wamealikwa kushiriki mashindano haya, walilemewa kwa mabao 2-0 na Brazil katika mechi ya kujipima nguvu wiki mbili zilizopita.

Walitoka 1-1 dhidi ya Paraguay kabla ya kulizwa na Colombia 1-0 katika mechi za makundi ya Copa America.

Argentina inatafuta ushindi wake wa kwanza katika makala haya ya 46 baada ya kupoteza dhidi ya Colombia na kugawana alama dhidi ya Paraguay.

Akizungumza baada ya Argentina kupata alama dhidi ya Paraguay, mshambuliaji wa Barcelona Messi alisema, “Lazima tuwe na fikra kuwa tuna uwezo wa kutosha. Tunastahili kujiamini.”

Aliongeza, “Tutahitajika kuimarika na kuwasili katika mechi ijayo tukiwa katika hali nzuri…lazima tuishinde.”

Mechi nyingine itakayosakatwa leo itakutanisha Ecuador na Japan.

Ecuador ililimwa 4-0 na Uruguay kwa hivyo iko katika ulazima wa kushinda iwapo inadhamiria kusalia mashindanoni.

You can share this post!

NUKSI TWAIKATAA: Stars yalenga kuondoa ‘swara’ Afcon

FUNGUKA: ‘Nikiona rinda mwili hutetema’

adminleo