• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
COPA AMERICA: Kiungo James Rodriguez atemwa kwenye kikosi cha Colombia

COPA AMERICA: Kiungo James Rodriguez atemwa kwenye kikosi cha Colombia

Na MASHIRIKA

KIUNGO James Rodriguez wa Everton amesema “anasikitishwa sana” na hatua ya kutemwa kwake kwenye kikosi kitakachotegemewa na Colombia kwenye fainali zijazo za Copa America.

Rodriguez pia hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Colombia kwenye mechi zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Hii ni baada ya Shirikisho la Soka la Colombia (CFF) kushikilia kwamba mwanasoka huyo wa zamani wa Real Madrid “hayuko katika fomu nzuri ya kuwajibishwa kwenye mapambano ya haiba kubwa yenye ushindani mkali”.

Hata hivyo, Rodriguez, 29, amesema kwamba anashangazwa sana na hatua hiyo.

“Yasikitisha sana iwapo benchi ya kiufundi inakosa imani nawe,” akasema Rodriguez.

Rodriguez alijiunga na Everton mnamo Septemba 2020 baada ya kuagana rasmi na Real. Hata hivyo, majeraha ya mara kwa mara yalimkosesha mechi kadhaa za msimu wa 2020-21 huku akiwajibishwa na kocha Carlo Ancelotti mara 23 pekee kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Rodriguez alikosa mechi mbili za mwisho zilizotandazwa na Everton msimu huu wa 2020-21 – ile iliyowashuhudia waajiri wake wakisajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Wolves ugani Goodison Park na iliyowapa mabingwa Manchester City jukwaa la kuwaponda 5-0 uwanjani Etihad.

Rodriguez anahisi kwamba iwapo fomu yake haitamwezesha kuongoza mashambulizi ya Colombia dhidi ya Peru mnamo Juni 4, basi atakuwa katika hali shwari ya kukiwajibikia kikosi chake dhidi ya Argentina katika mchuano mwingine wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia siku tano baadaye.

Kivumbi cha Copa America kimeratibiwa kufanyika kati ya Juni 13 na Julai 10. Colombia walikuwa washirikiane na Argentina kuwa waandalizi wa pamoja wa kipute hicho lakini wakapokonywa fursa hiyo baada ya maandamano ya raia dhidi ya serikali kuzuka nchini humo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jesse Were asherehekea kufikisha mabao 100 Zesco United...

Mbinu mbalimbali za kuimarisha kinga mwilini