Arsenal kuanza mazoezi chini ya masharti makali
Na CHRIS ADUNGO
WACHEZAJI wa Arsenal wamepangiwa kurejea kambini kuanza mazoezi katika uwanja wa London Colney, Uingereza kwa minajili ya mechi zilizosalia katika kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mazoezi hayo yanatarajiwa kuendeshwa kwa mujibu wa kanuni za serikali kuhusu jinsi ya kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona.
“Wachezaji wataruhusiwa kufanyia mazoezi katika uwanja wa London Colney. Idadi ya watakaokuwa wakitumia uwanja huo kwa wakati mmoja itadhibitiwa huku mazoezi yakiendeshwa kwa utaratibu utakaoshuhudia wachezaji wakidumisha umbali wa mita moja kati yao,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Arsenal.
“Majengo yote yaliyoko katika eneo la Colney yatafungwa na wachezaji watahitajika kusafiri mmoja mmoja katika magari yao binafsi. Baada ya kila mmoja kukamilisha vipindi vyake vya mazoezi, atatakiwa kurejea nyumbani moja kwa moja,” ikaongeza taarifa hiyo.
Hatua hiyo ya Arsenal inachukuliwa na Arsenal siku mbili tu baada ya usimamizi kuandaa kikao cha dharura na wachezaji wote kufuatia kisa ambapo Alexandre Lacazette, David Luiz, Nicolas Pepe na Granit Xhaka walipatikana na hatia ya kukiuka kanuni ya kuwa mbali kwa mita moja na zaidi.
Lacazette ambaye anahusishwa na uwezekano wa kutua Uhispania kuchezea Barcelona alionekana akiwa karibu sana na mtu aliyekuwa akiliosha gari lake. Kwa upande wao, Luiz na Xhaka walionekana wakikaribiana sana walipokuwa wakiponda raha katika bustani moja jijini London huku Pepe akionekana akicheza mpira na baadhi ya marafiki zake.
Wanne hao walionywa huku usimamizi wa Arsenal ukiapa kutoa adhabu kali zaidi kwa mwanasoka wao yeyote atakayekiuka kanuni ambazo zimewekwa na serikali ya Uingereza kukabiliana na corona.
Kwa mujibu wa serikali ya Uingereza, mchezaji yeyote anaruhusiwa kushiriki mazoezi kivyake au kwa pamoja na watu anaoishi nao nyumba moja baada ya wao wote kufanyiwa vipimo vya afya kubaini iwapo wana virusi vya corona au la.
Na iwapo mchezaji atataka kujifanyia mazoezi nje ya makazi yake, kanuni ni kwamba atahitajika kudumisha umbali wa hadi mita mbili au futi sita kati yake na mtu yeyote mwingine.
Kivumbi cha EPL kinatarajiwa kurejelewa chini ya kipindi cha wiki chache zijazo baada ya vinara wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kufichua mipango ya kuanza upya kipute hicho mnamo Mei 9.
Tayari vikosi vyote 18 vinavyowania ufalme wa Bundeliga msimu huu vimekita kambi chini ya mwongozo wa kanuni kali kuhusu afya.