• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Arsenal waambulia sare ya 1-1 dhidi ya Southampton ligini

Arsenal waambulia sare ya 1-1 dhidi ya Southampton ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amesema kwamba sare ya 1-1 iliyosajiliwa na kikosi chake dhidi ya Southampton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatano usiku ni ishara ya ufufuo mkubwa wa kikosi chake.

Arsenal walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo uwanjani Emirates wakiwa na rekodi mbovu ya kupoteza mechi tatu mfululizo za ligi.

Theo Walcott aliwaweka Southampton kifua mbele katika dakika ya 18 baada ya kumzidi maarifa kipa Bernd Leno.

Hata hivyo, Pierre-Emerick Aubameyang alisawazishia Arsenal katika dakika ya 52 na kukomesha ukame wa dakika 797 bila mabao katika soka ya EPL tangu afunge penalti katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester United mnamo Novemba 1, 2020.

Ingawa bao hilo lilitarajiwa kurejesha Arsenal mchezoni na kuwapa motisha ya kuzamisha kabisa chombo cha Southampton, vijana wa Arteta walipatwa na pigo baada ya Gabriel Magalhaes kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 62.

Kupunguzwa kwa idadi ya wachezaji wa Arsenal kuzidisha ari ya Southampton walioshuhudia kombora la Nathan Redmond likigonga mwamba wa goli la wenyeji wao katika dakika ya 77. Ushindi kwa Southampton ungaliwashuhudia wakipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 26, mbili nyuma ya viongozi Liverpool waliowacharaza Tottenham Hotspur 2-1 ugani Anfield.

Arsenal kwa upande wao walisalia katika nafasi ya 15 kwa alama 14, hii ikiwa rekodi duni zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kushuhudia tangu 1974-75.

Arsenal walianza mchuano huo kwa matao ya juu huku ushirikiano mkubwa kati ya Aubameyang, Eddie Nketiah na Bukayo Saka ukiwatatiza mabeki wa Southampton.

Kadi nyekundu ambayo Gabriel alionyeshwa ilikuwa ya saba kwa kikosi cha Arsenal kuonyeshwa katika EPL tangu Arteta apokezwe mikoba ya kikosi hicho mnamo Disemba 2019. Aidha, hiyo ilikuwa kadi ya tatu nyekundu kwa Arsenal kuonyeshwa kutokana na mechi tano zilizopita baada ya Nicolas Pepe na Granit Xhaka kufurushwa uwanjani kwa utovu wa nidhamu katika mechi za awali dhidi ya Leeds United na Burnley.

Arsenal hawajawahi kushinda mchuano wowote wa EPL msimu huu tangu wapepete Man-United 1-0 uwanjani Old Trafford wiki sita zilizopita. Arteta aliyepanga kikosi kichanga zaidi cha Arsenal dhidi ya Southampton tangu Septemba 2012, ni mwingi wa matumaini kwamba kikosi chake kitafufua makali na kujikweza pazuri zaidi jedwalini.

Mechi dhidi ya Southampton ilikuwa ya 50 kwa Arteta kusimamia kambini mwa Arsenal ambao amewaongoza kushinda idadi kubwa zaidi ya michuano kwenye mashindano ya makombe mengine (14) kuliko EPL (13).

Arsenal kwa sasa wana kibarua kigumu cha kukabiliana na Everton, Chelsea, Manchester City na Brighton katika kipindi cha siku 10 zijazo kabla ya kufungwa kwa kampeni za mwaka huu wa 2020. Kwa upande wao, Southampton wataalika Manchester City uwanjani St Mary’s mnamo Disemba 19.

You can share this post!

Fida yawashikisha adabu Aisha Jumwa na Edwin Sifuna

Mambo yaenda segemnege