Michezo

Arsenal wazamisha chombo cha Fulham katika EPL

September 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

SAJILI wapya Gabriel Magalhaes na Willian Borges waliwapa mashabiki na waajiri wao Arsenal sababu za kutabasamu na kutarajia makuu zaidi kutoka kwao katika kampeni za msimu huu nchini Uingereza na bara Ulaya.

Wawili hao walikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza kilichotegemewa jana na kocha Mikel Arteta katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililowashuhudia Arsenal wakiwapepeta Fulham 3-0 uwanjani Craven Cottage.

Willian, ambaye alisajiliwa kutoka Chelsea bila ada yoyote mwezi uliopita, alichangia mabao yote matatu ya Arsenal huku Gabriel aliyeagana na Lille ya Ufaransa kwa Sh3.2 bilioni akitikisa nyavu za wapinzani.

Arsenal walianza mchuano huo kwa matao ya juu na kuvamia lango la wenyeji wao kuanzia dakika ya kwanza. Ushirikiano mkubwa kati ya Willian na beki Hector Bellerin ulichangia bao la kwanza la Arsenal lililojazwa kimiani na fowadi Alexandre Lacazette katika dakika ya nane kabla ya Gabriel kufunga la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Bao la Gabriel lilitokana na kona iliyochanjwa na Willian ambaye alishuhudia kombora lake likigonga mhimili wa goli kabla ya kutoa krosi iliyofumwa kimiani na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang kunako dakika ya 57.

Fulham walikuwa na fursa chache za kutatiza mabeki wa Arsenal katika gozi hilo huku nafasi nzuri zaidi waliyoipata ikitokea katika dakika ya 27. Hata hivyo, fowadi wao tegemeo aliyeibuka mfungaji bora msimu jana, Aleksandar Mitrovic, aliipoteza nafasi hiyo ya wazi licha ya kusalia uso kwa macho na kipa Bernd Leno.

Arsenal walionyesha ishara nyingi za kuimarika chini ya kocha Arteta ambaye kwa sasa amesuka upya kikosi kilichobana vizuri safu ya ulinzi na kuvamia wapinzani kwa kasi zaidi kila mara viungo walipopata mpira.

Chini ya mkufunzi huyo mzawa wa Uhispania aliyewahi kuwa mchezaji wao, Arsenal waliwabwaga Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mwishoni mwa msimu uliopita kabla ya kuwaangusha Liverpool kwenye Community Shield mwanzoni mwa muhula huu.

Dani Ceballos na Eddie Nketiah waliovurugana nje ya uwanja kabla ya mchuano huo kuanza waliingia ugani katika kipindi cha pili kujaza nafasi za Granit Xhaka na Lacazette mtawalia.

Fulham walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara huku ushirikiano mkubwa kati ya Ainsley Maitland-Niles, Kieran Tierney, Bellerin na Gabriel kwenye safu ya nyuma ukiwapa washambuliaji wa kocha Scott Parker kibarua kigumu.

Mohamed Elneny na Xhaka ambao dalili zote ziliashiria kwamba msimu uliopita ungalikuwa wao wa mwisho kambini mwa Arsenal, pia waliridhisha pakubwa kwenye safu ya kati.

Leno alianzishwa kwenye lango, kuashiria kwamba kipa Emiliano Martinez aliyetegemewa sana na Arsenal mwishoni mwa muhula jana, yuko pua na mdomo kubanduka ugani Emirates.

Kwa msimu wa nne mfululizo, ilichukuwa muda wa chini ya dakika 10 kwa bao la kwanza katika msimu mpya wa kampeni ya EPL kupatikana. Lacazette sasa anakuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la kwanza kwenye misimu miwili tofauti ya EPL.

Gabriel anakuwa beki wa tatu wa Arsenal kufunga bao katika mchuano wake wa kwanza wa EPL huku Willian akiweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kuchangia mabao matatu ya Arsenal katika mechi yake ya kwanza tangu Ray Parlour mnamo Agosti 1992 dhidi ya Liverpool.

Fulham walishushwa ngazi kwenye EPL mnamo 2013-14 na 2018-19 baada ya kufunga idadi kubwa ya mabao. Mara ya mwisho walipopandishwa daraja kushiriki EPL, walitumia zaidi ya Sh14 bilioni kusuka kikosi kipya kilichoshindwa kuhimili ushindani mkali kwenye soka ya Uingereza.