• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:27 AM
Arsenal yaikandamiza Manchester City nusu-fainali ya Kombe la FA

Arsenal yaikandamiza Manchester City nusu-fainali ya Kombe la FA

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Mikel Arteta alimzidi maarifa mwelekezi wake Pep Guardiola katika mechi ya nusu-fainali ya Kombe la FA iliyowashuhudia Arsenal wakiwapepeta Manchester City 2-0 uwanjani Wembley, London mnamo Julai 18, 2020.

Arteta alibanduka rasmi uwanjani Etihad alikokuwa msaidizi wa Guardiola mnamo Disemba 2019 na kutua uwanjani Emirates kudhibiti mikoba ya Arsenal ambao pia waliwahi kujivunia huduma zake akiwa mchezaji.

Kuajiriwa kwake na Arsenal kulichochewa na haja ya kujaza pengo la mkufunzi Unai Emery aliyetimuliwa kwa msururu wa matokeo duni.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Arsenal akiwa kocha, Arteta kwa sasa ana fursa ya kukitwalia kikosi hicho taji muhimu msimu huu atakapowaongoza kunogesha fainali ya Kombe la FA dhidi ya mshindi wa nusu-fainali ya pili itakayowakutanisha leo Manchester United na Chelsea.

Mshambuliaji na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang aliwaweka Arsenal kifua mbele kunako dakika ya 19 kabla ya kukizamisha kabisa chombo cha Man-City katika dakika ya 71 alipomwacha hoi kipa Ederson Moraes.

Bao hilo la pili la Aubameyang lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na beki Kieran Tierney huku la kwanza likichangiwa na fowadi mahiri wa Ivory Coast, Nicolas

Man-City ambao ni washikilizi wa Kombe la FA, walirejea uwanjani kwa minajili ya kipindi cha pili kwa matao ya juu huku wakimiliki asilimia kubwa ya mpira, kuwatamalaki wapinzani wao na kulishambulia sana lango la kipa Emiliano Martinez.

Ushindi huo wa Arsenal ambao kwa sasa wanajivunia ufufuo mkubwa chini ya Arteta, uliwajia siku tatu pekee baada ya kuwapokeza Liverpool kichapo cha 2-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Emirates mnamo Julai 15, 2020.

Kinyume na alivyokuwa katika mchuano wa kwanza dhidi ya Man-City tangu kurejelewa kwa soka ya Uingereza msimu huu, beki David Luiz alikuwa makini zaidi na aliidhibiti vilivyo safu ya ulinzi ya Arsenal ambayo kwa sasa itakosa huduma za Mjerumani Shkodran Mustafi aliyepata jeraha la paja mwishoni mwa kipindi cha pili.

Wanapojiandaa kwa fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1, 2020, Arsenal watapania pia kufukuzia nafasi ya kufuzu kwa kivumbi cha Europa League msimu ujao. Kwa sasa wanashikilia nafasi ya 10 kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 53 na wamepangiwa kuvaana na Aston Villa na Watford katika michuano miwili ya mwisho wa msimu huu ligini.

Arsenal ndio wanaoshikilia rekodi ya kujizolea ufalme wa Kombe la FA kwa mara nyingi zaidi (mara 13). Walifuzu kwa nusu-fainali za kivumbi hicho msimu huu kwa kuwapepeta Sheffield United 2-1 uwanjani Bramall Lane mnamo Juni 28, 2020.

Mabao yao wakati huo yalimiminwa kimiani kupitia kwa fowadi Nicolas Pepe aliyefunga penalti ya kipindi cha kwanza kabla ya Dani Ceballos kucheka na nyavu mwishoni mwa kipindi cha pili.

Nusu-fainali ya leo Jumapili kati ya Man-United na Chelsea ni marudio ya fainali ya Kombe la FA mnamo 2018 iliyoshuhudia Chelsea wakiibuka na ushindi wa 1-0 ugani Wembley.

You can share this post!

JAMVI: Ishara zajitokeza Moi ndiye mrithi wa Uhuru 2022

Makanisa yatumia teknolojia kusajili waumini kwa ibada

adminleo