Michezo

Arsenal yapata afueni ratiba ya EPL ikigeuzwa

April 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

LONDON, Uingereza

Mechi kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza zimesukumwa mbele siku moja zikiwemo za farasi watatu Arsenal, Liverpool na Manchester City kwa ajili ya kupeperushwa moja kwa moja kwenye runinga.

Wanabunduki wa Arsenal na mashetani wekundu wa Manchester United walifaa kuvaana Mei 11 ugani Old Trafford, lakini sasa watafanya hivyo Mei 12 baada ya kutiwa katika orodha ya mechi zitakazoonyeshwa na runinga ya Sky.

Hii inatoa fursa kwa Arsenal ya kocha Mikel Arteta kupumzika siku moja zaidi baada ya mchuano wao na Bournemouth hapo Mei 4.

Soma pia: Nipe nikupe: Arsenal warusha chini Man City na kurejea tena juu ya mti wakisubiri jibu la Liverpool

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp sasa itakabana koo na Aston Villa ugani Villa Park mnamo Mei 13 kabla ya mabingwa watetezi Manchester City kupimana makali na Tottenham Hotspur mnamo Mei 14.

Raundi ya mwisho ya mechi za Ligi Kuu ni Mei 19 wakati shughuli itaanza saa kumi na mbili jioni katika viwanja vyote.

Arsenal wamekaa juu ya jedwali kwa alama 71, mbele ya Liverpool kwa ubora wa magoli na alama moja mbele ya City.

Inamaanisha kuwa ligi inaweza kuamuliwa siku ya mwisho farasi hao wasipoteleza katika mechi sita zijazo ligini.

Arsenal watafunga msimu dhidi ya Everton ugani Emirates, Liverpool watazichapa na Wolves uwanjani Anfield nao City wataalika West Ham ugani Etihad.

Soma pia: Arsenal inayomhemea beki Kimmich wa Bayern yaambiwa ‘tuongee baada ya kazi’

        Wachanganuzi washikilia ‘Ndovu’ Arsenal hawatabeba taji la EPL licha ya sare na Man City