Arteta imani tele Aubameyang atarefusha mkataba Arsenal
Na CHRIS ADUNGO
KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amesema ana imani kubwa kwamba mashambuliaji na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang atatia saini mkataba mpya uwanjani Emirates.
Nyota huyo mzawa wa Gabon alifunga mabao mawili katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na Arsenal dhidi ya Norwich City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Julai 1, 2020 ugani Emirates.
Aubameyang kwa sasa ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Arsenal kuwahi kufikisha idadi ya mabao 50 ya EPL haraka zaidi katika historia ya kikosi hicho.
Anajivunia kufungia Arsenal jumla ya mabao 51 kutokana na mechi 79 zilizopita za EPL na kwa sasa anapigiwa upatu wa kuibuka mfungaji bora wa soka ya Uingereza kwa msimu wa pili mfululizo.
Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba jedwalini kwa alama 46, tisa nyuma ya Leicester City wanaofunga orodha ya tatu-bora.
Bao la kwanza la Arsenal ambalo lilifumwa wavuni na Aubameyang kunako dakika 33 lilikuwa zao la masihara ya kipa mzawa wa Uholanzi, Tim Krul aliyeshindwa kuondoa mpira katika kijisanduku chake.
Bao la pili la Arsenal lilipachikwa wavuni na kiungo Granit Xhaka aliyeshirikiana vilivyo na Aubameyang kunako dakika ya 37. Goli hilo la Xhaka lilikuwa lake la kwanza tangu Machi 2019.
Arsenal walifungiwa bao la tatu kupitia kwa Aubameyang aliyemwacha hoi beki Josip Drmic kunako dakika ya 67 kabla ya beki Cedric Soares kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao dakika tisa kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa.
Soares alivurumisha kombora kutokea nje ya msambamba dakika nne pekee baada ya kutokea benchi katika kipindi cha pili.
Zikisalia mechi sita pekee kabla ya kampeni za msimu huu kutamatika rasmi, Norwich kwa sasa wanakokota nanga mkiani mwa jedwali kwa alama 21.
Baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza tangu kurejelewa kwa kipute cha EPL dhidi ya Manchester City na Brighton, Arsenal kwa sasa wamesajili ushindi katika michuano mitatu iliyopita na wametinga nusu-fainali ya Kombe la FA ambapo watakutana na Man-City uwanjani Wembley mnamo Julai 18, 2020.
Mabao mawili yaliyofungwa na Aubameyang mnamo Julai 1 dhidi ya Norwich kwa sasa yanamweka katika nafasi moja na Jamie Vardy wa Leicester City anayeongoza orodha ya wafungaji bora ya EPL hadi kufikia sasa muhula huu. Wawili hao wamepachika wavuni magoli 19 kila mmoja.
Norwich kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Brighton uwanjani Carrow Road kabla ya kuwaendea Watford ugani Vicarage Road kisha kuwaalika West Ham United kwa usanjari huo. Kwa upande wao, Arsenal watakuwa wageni wa Wolves mnamo Jumamosi ya Julai 4, 2020.
MATOKEO YA EPL (Julai 1):
Arsenal 4-0 Norwich City
Bournemouth 1-4 Newcastle
Everton 2-1 Leicester City
West Ham United 3-2 Chelsea