ATATOBOA PRESHA? Maguire ajue mashabiki wana matarajio makubwa kwake
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
MLINZI wa kimataifa, Virgil van Dijik wa klabu ya Liverpool amemuonya Harry Maguire kwamba kiasi kikubwa cha pesa kilichotumiwa kumsajili kitawafanya mashabiki wa Manchester United kuwa na matarajio mengi kutoka kwake.
Manchester United imemsajili Maguire kwa kiasi cha Sh10 bilioni ambacho kimevunja rekodi ya Dijik ya Sh9.4 bilioni kilichotumiwa na Liverpool kumng’oa Southampton.
Maguire ambaye msimu uliopita aliichezea Leicester City anatarajiwa kuwa tegemeo kwenye kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer kitakachovaana na Chelsea Jumapili, lakini atatakiwa kujituma zaidi uwanjani kuthibitisha thamani yake.
“Twamtakia kila la heri,” alisema. “Siwezi kusema chochote kuhusu rekodi yangu kuvunjwa kwa sababu nilijua wakati mmoja itavunjwa. Sina uwezo wa kuzungumza zaidi, lakini namtakia kila la heri. Hata hivyo, ningependa kumfahamisha kuwa pesa nyingi zina changamoto zake hasa unapochezea klabu kubwa kama Man United.”
Alipoulizwa alivyoweza kukabiliana na changamoto kama hizo, Van Dijk alisema: “Muhimu ni kuwa na lengo kwa lolote unalofanya uwanjani na kucheza kuliko uwezo wako, furahia mchezo wako na usifikirie kuhusu mambo mengine unapokuwa uwanjani. Sio rahisi kuhimili presha ya mashabiki. Binafsi napenda kucheza kwa bidii. Ni muhimu kujitolea muhanga unapokuwa uwanjani.”
Baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa EPL tangu 1990 walipokuwa chini ya kocha Kenny Dalglish, Van Dijk aliongoza Liverpool kumaliza ligi katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City kwa tofauti ya pointi moja pekee.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 amekubali mkataba wa miaka sita katika uwanja wa Old Trafford, huku akiwa na fursa ya kuongeza mwaka mmoja.
“Wakati Man United inapoanza kukuulizia, ni fursa nzuri”, alisema Maguire.
Maguire ndiye mchezaji wa pili ghali zaidi kusainiwa katika ligi ya Uingereza baada ya Paul Pogba aliyejiunga na Man United kwa dau la Sh13.3 bilioni na amekuwa mchezaji wa pili ghali wa Uingereza baada ya winga wa Wales Gareth Bale, ambaye alijiunga na Real Madrid kutoka Tottenham kwa dau la Sh12.7 bilioni mnamo 2013.
Mchezaji wa tatu
Ni mchezaji wa tatu kusajiliwa na kocha Ole Gunnar Solskjaer, baada ya Aaron wan Bissaka kutua kutoka Crystal Palace kwa dau la Sh7.5 bilioni wakati winga Daniel James akijiunga na miamba hiyo kutoka Swansea kwa dau la Sh2.2 bilioni.
Maguire aliongezea: kufuatia mazungumzo yetu na mkufunzi, ninafurahia kuhusu maono na mipango aliyonayo kwa timu. Ni wazi kwamba Ole anajenga timu itakayoshinda mataji.
Kwa sasa nataraji kukutana na wachezaji wenzangu kabla ya msimu kuanza.
Solskjaer: “Harry ni miongoni mwa wachezaji bora katika mchezo huu leo. Anajua kusoma mchezo na uwepo wake katika uwanja unaonekana huku akiwa na uwezo wa kutulia kunapotokea shinikizo.”