Michezo

Atletico wapiga Barcelona na kufikia Real Sociedad kileleni mwa jedwali la La Liga

November 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ATLETICO Madrid walipiga Barcelona 1-0 na kupaa hadi kileleni mwa jedwalini kwa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 20 sawa na viongozi Real Sociedad.

Ushindi uliosajiliwa na Atletico uliwasaza Barcelona katika nafasi ya 10 kwa alama 11 sawa na Valencia, Getafe na Osasuna. Ni pengo la pointi tisa ambalo kwa sasa linatamalaki kati ya Barcelona na viongozi wawili wa jedwali la La Liga.

Yannick Carrasco ndiye alikuwa mfungaji wa bao la pekee na la ushindi dhidi ya Barcelona mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kumwacha hoi kipa Marc-Andre ter Stegen.

Pigo kubwa zaidi kwa Barcelona ni jeraha alilolipata beki Gerard Pique aliyelazimika kuondoka uwanjani katika kipindi cha pili.

Kwa mujibu wa Barcelona, Pique alipata jeraha la goti la kulia na sasa wanasubiri tathmini zaidi ya madaktari ili kubaini urefu wa muda atakaohitaji mkekani kuuguza jeraha hilo.

Ingawa hivyo, kocha Ronald Koeman amefichua kwamba huenda nyota huyo akalazimika kusalia nje kwa kipindi cha miezi sita kabla ya kurejea ugani.

Barcelona walionekana kuzidiwa maarifa kwenye takriban kila idara katika mchuano huo huku jaribio lao la pekee langoni pa Atletico kupitia kwa Clement Lenglet likidhibitiwa vilivyo na kipa Jan Oblak.

Barcelona kwa sasa wamejizolea alama 11 pekee kutokana na mechi nane za La Liga, tisa nyuma ya Sociedad ambao wameorodheshwa mbele ya Atletico kutokana na wingi wa mabao ambayo wamefunga.

Kichapo ambacho Barcelona walipokea kiliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Atletico hadi kufikia sasa msimu huu na wanajivunia kutopigwa katika jumla ya mechi 24 zilizopita kwenye mashindano yote. Kwa upande wao, hicho kilikuwa kichapo cha tatu kwa Barcelona kupokezwa kutokana na mechi nane zilizopita za La Liga.

Nyota Lionel Messi aliyepangwa katika kikosi cha akiba cha Barcelona hakuchezeshwa dhidi ya Atletico ikizingatiwa kwamba alikuwa tu amerejea kambini mwa miamba hao wa Uhispania baada ya kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Argentina kwenye mechi za kimataifa za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

“Ulikuwa wakati wetu kushinda na hatutaruhusu sifa ambazo tutamiminiwa na vyombo vya habari kutokana na ushindi huo kutupotezea dira. Malengo yetu ya msimu huu yako dhahiri na tuko tayari kupigana hadi mwisho,” akatanguliza kocha Diego Simeone wa Atletico.

“Tuliingia ugani tukijua cha kufanya katika safu ya ulinzi ili kuzuia mashambulizi ya Barcelona na safu ya mbele ili kutatiza mabeki wao. Tulifaulu katika mpango wetu,” akaongeza raia huyo wa Argentina.

Kwa upande wake, Koeman alisema: “Kikosi cha haiba kubwa kama Barcelona hakiwezi kufungwa bao la kiaibu namna hiyo. Wachezaji walizembea na wakafanya masihara mengi katika kila idara. Hatuwezi kuruhusu utepetevu wa aina hiyo kuendelea kikosini.”

Mkufunzi huyo amewahi kuinoa timu ya taifa ya Uholanzi na klabu ya Everton.