Michezo

Aubameyang kusaidia Arsenal kufuma mabao hadi 2023

September 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI na nahodha wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, 31, ametia saini mkataba mpya wa miaka mitatu uwanjani Emirates.

Sogora huyo raia wa Gabon alijiunga na Arsenal mnamo Januari 2018 baada ya kuagana na Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa kima cha Sh7.8 bilioni.

Atakuwa sasa akipokezwa mshahara wa Sh35 milioni kwa wiki.

Katika msimu wake wa kwanza mkamilifu kwenye soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), alipachika wavuni jumla ya mabao 23 na akatawazwa mfungaji bora kwa pamoja na Sadio Mane na Mohamed Salah wa Liverpool.

“Suala la kurefusha mkataba kambini mwa Arsenal halikuwa na shaka. Naamini kikosi cha sasa cha Arsenal na tuna uwezo wa kujivunia mambo mengi. Nahisi kwamba tuna kitu kizuri cha kuipa klabu hii na mambo mazuri zaidi yako karibu kufanyikia timu hii,” akasema.

Mkataba wa Aubameyang na Arsenal ulitarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21, kumaanisha kwamba angalikuwa huru kusaka hifadhi mpya mwanzoni mwa Januari 2021.

Hadi aliporefusha muda wa kuhudumu kwake ugani Emirates, Aubameyang alikuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Real Madrid, Barcelona, Juventus, Inter Milan na Chelsea.

Nyota huyo alifunga bao la pili la Arsenal katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Fulham katika mchuano wa kwanza wa EPL msimu huu mnamo Septemba 12, 2020 uwanjani Craven Cottage.

Aidha, alifungia Arsenal mabao mawili kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea mnamo Agosti 1, 2020 na kuipa klabu hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta fursa ya kunogesha kipute cha Europa League mnamo 2020-21.

“Ilikuwa vyema na muhimu zaidi kwa Aubameyang kusalia nasi. Ni mchezaji wa haiba kubwa aliye na uwezo mkubwa ndani na nje ya uwanja. Kuweka historia ya kuwa mwanasoka wa kwanza kufunga mabao 50 haraka zaidi katika kikosi hiki kikubwa si jambo dogo,” akasema Arteta.

“Aubameyang ni kiongozi muhimu kwa Arsenal na sehemu kubwa ya mpango wetu wa kujisuka upya. Anatamani kuwa huko juu pamoja na wanasoka wengine wa haiba kubwa duniani ilia ache taathira za kudumu katika ulingo wa soka,” akaongeza Arteta.

Tangu ajiunge na Arsenal, Aubameyang amefungia waajiri wake jumla ya mabao 72 katika mechi 111 kwenye mashindano yote. Katika mechi 86 za EPL, amepachika wavuni mabao 55 na kuchangia mengine 12.

Mshindi huyo wa taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka 2015 barani Afrika alipokezwa utepe wa unahodha wa Arsenal mnamo Novemba 2019 baada ya mtangulizi wa Arteta, kocha Unai Emery kumvua kiungo Granit Xhaka unahodha wa kikosi.

Kufikia sasa, Arsenal wamesajili wanasoka Gabriel Magalhaes kutoka Lille, Willian kutoka Chelsea na Dani Ceballos aliyerefusha kipindi chake mkopo kwa mwaka mmoja zaidi kutoka Real Madrid.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO