• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 10:59 AM
Aubameyang yuko karibu kutia saini mkataba mpya Arsenal

Aubameyang yuko karibu kutia saini mkataba mpya Arsenal

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal ni mwingi wa matumaini kwamba nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, 31, atatia saini mkataba mpya.

Aubameyang ambaye ni mshambuliaji mzawa wa Gabon, alijiunga na Arsenal mnamo Januari 2018 baada ya kuagana na Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Kwa sasa amesalia na mwaka mmoja pekee kwenye kandarasi yake na Arsenal ambao chini ya Arteta, wamepania kumpokeza mshahara wa hadi Sh35 milioni kwa wiki ili kumshawishi arefushe muda wa kuhudumu kwake ugani Emirates.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri na Aubameyang na wakala wake. Nina imani tele kwamba tutaafikiana hivi karibuni. Hivyo ndivyo ninavyohisi,” akasema Arteta.

Aidha, Arteta amefichua kwamba anatarajia beki Gabriel Magalhaes wa Lille arasimishe uhamisho wake hadi Arsenal hivi karibuni.

Arsenal wamekuwa wakimvizia beki huyo mzawa wa Brazil mwenye umri wa miaka 22 kwa kipindi kirefu sasa na magazeti mengi nchini Uingereza yameripoti kwamba tayari amefanyiwa vipimo vya afya uwanjani Emirates mwanzoni mwa wiki hii.

Arteta, ambaye ni nahodha wa zamani wa Arsenal, aliteuliwa kuwa mrithi wa kocha Unai Emery ugani Emirates mnamo Disemba 2019.

“Hatuwezi kutangaza chochote kwamba ni rasmi kwa sasa. Mambo ya Aubameyang na Magalhaes bado yatasubiri kidogo japo nina kila sababu ya kutumainia mazuri,” akasema Arteta.

“Mara nyingine hatua za mwisho katika kufanikisha mambo ndiyo huwa ngumu zaidi. Tunatarajia ripoti nzuri hata hivyo na hivi karibuni tutafichua matokeo ya mazungumzo marefu tukayoandaa wiki hii,” akaongeza.

Arsenal walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2019-20 katika nafasi ya nane. Hata hivyo, walifuzu kwa kipute cha Europa League msimu ujao kwa pamoja na Leicester City na Tottenham Hotspur.

Hii ni baada ya Arteta kuwaongoza Arsenal kupepeta Chelsea 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA iliyoshuhudia Aubameyang akifunga mabao yote mawili ya waajiri wake ugani Wembley, Uingereza.

You can share this post!

Uchafu Mto Ngong waharibu sifa ya Nairobi

Kipa Henderson kuwadakia Man-United hadi Juni 2025