Michezo

Australia, New Zealand kuandaa fainali za Kombe la Dunia soka ya wanawake 2023

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

AUSTRALIA na New Zealand sasa watakuwa wenyeji wa pamoja wa fainali za Kombe la Dunia za Soka ya Wanawake mnamo 2023.

Wawili hao walipiku Colombia waliokuwa wawaniaji wengine wa fursa ya kuandaa kivumbi hicho baada ya Brazil na Japan kujiondoa mwanzoni mwa Juni 2020 kutokana na janga la corona.

Kwa mara ya kwanza, makala ya 2023 yatashirikisha vikosi 32 badala ya 24 vilivyokuwa vikinogesha fainali hizo katika miaka ya awali.

Fainali hizo za Kombe la Dunia zimepangiwa kufanyika kati ya Julai na Agosti 2023.

“Mchakato wa kutafuta mwandalizi mpya ulikuwa na ushindani mkali. Tunashukuru Australia na New Zealand kwa kuipata fursa hiyo, japo tunatambua pia ukubwa wa uwezo wa Colombia waliokuwa wakipigiwa upatu na Brazil ambao walikuwa wawe wenyeji rasmi,” akasema Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino.

Kwa pamoja, Australia na New Zealand walipata jumla ya kura 22 kutokana na 35 zilizopigwa na wanachama wa Baraza Kuu la FIFA. Colombia walijizolea kura 13 pekee. Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), Greg Clarke alipigia kura Colombia.

Infantino ametangaza pia kupigwa jeki kwa juhudi za waandalizi wa fainali hizo za Kombe la Dunia kifedha.

“FIFA imetoa pia jumla ya Sh112 bilioni ambazo zitapokezwa mashirikisho wanachama kwa minajili ya maendeleo ya soka ya wanawake kote ulimwenguni katika kipindi cha miaka minne ijayo,” akatanguliza.

“Tulishuhudia fainali za kuridhisha sana za soka ya wanawake mwaka jana nchini Ufaransa. Ni kipute kilichovunja rekodi kwa jinsi kilivyofikisha soka ya wanawake hadi kiwango kingine tofauti kabisa na cha juu zaidi duniani,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba hawatarijii chochote kitakachopungua kiwango kilichoshuhudiwa Ufaransa wakati wa fainali za 2023.

Fainali za 2023 zitakuwa za kwanza kuwahi kuandalia na mashirikisho ya soka katika mabara mawili tofauti kwa kuwa Australia inapatikana bara Asia na New Zealand inapatikana Oceania.

Kwa pamoja na Chris Nikou ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la Australia (FFA), Johanna Wood ambaye ni Rais wa Shirikisho la Soka la New Zealand, wameahidi kushirikiana vilivyo na kufanikisha maandalizi ya fainali za kufana mnamo 2023.

VIWANJA 8 VITAKAVYOTUMIKA AUSTRALIA:

Australia, Sydney (fainali): mashabiki 70,000

Sydney Football: mashabiki 42,512

Melbourne Rectangular: mashabiki 30,052

Brisbane: mashabiki 52,263

Perth Rectangular: mashabiki 22,225

Hindmarsh Adelaide: mashabiki 18,435

Newcastle: mashabiki 25,945

York Park, Launceston, Tasmania: mashabiki 22,065

VIWANJA 5 VITAKAVYOTUMIKA NEW ZEALAND:

Eden Park, Auckland (mechi ya ufunguzi): mashabiki 48,276

Wellington: mashabiki 39,000

Christchurch: mashabiki 22,556

Waikato Hamilton: mashabiki 25,111

Dunedin: mashabiki 28,744