Baada ya kuitia adabu Singida, Gor sasa kumenyana na Simba fainali
Na GEOFFREY ANENE
MEDDIE Kagere ameongoza Gor Mahia kutinga fainali yake ya pili mfululizo kwenye Soka ya SportPesa Super Cup baada ya kuisaidia kubwaga Singida United ya Tanzania 2-0 uwanjani Afraha mjini Nakuru, Alhamisi.
Katika uwanja telezi ulioanza kupondwa na mvua baada tu ya mchuano huu kuanza, mshambuliaji kutoka Rwanda, Kagere, alicheka na nyavu mara moja katika kila kipindi.
Aliwapa mabingwa watetezi Gor bao la ufunguzi dakika ya 35 alipokamilisha kwa ustadi kona safi kutoka kwa Francis Kahata kupitia kichwa chake.
Bao hili liliwasili sekunde chache baada ya Singida kugonga mwamba kupitia Deus Kaseke alivuta kiki zito kutoka nje ya kisanduku.
Gor ilipata nafasi nyingine nzuri dakika ya 72, lakini kipa Peter Manyika alikuwa macho kupangua shuti la George ‘Blackberry’ Odhiambo aliyekuwa amepokea krosi nzuri kutoka kwa Kahata.
Huku Singida, ambayo ilibandua nje AFC Leopards katika robo-fainali, ikitafuta bao la kusawazisha, Kagere alizima matumaini Watanzania hao kurejea mechini aliposukuma kombora nzito hadi wavuni dakika ya 90.
Gor sasa itakutana na Simba SC kutoka Tanzania katika fainali Juni 10. Itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba kati ya Kakamega Homeboyz (Kenya) na Singida (Tanzania).
Simba iliibandua Homeboyz nje kupitia mikwaju ya penalti 5-4 katika mechi ya nusu-fainali iliyotanguliwa kusakatwa uwanjani Afraha.
Mshindi kati ya mafahali Gor na Simba atazawadiwa Sh2 milioni na kunyakua tiketi ya kuenda nchini Uingereza kupambana na Everton uwanjani Goodison Park. Nambari mbili atatunikiwa Sh1 milioni.
Mwaka 2017, Gor ililemea Leopards 3-0 katika fainali jijini Dar es Salaam kabla ya kuchapwa 2-1 na Everton.