Bao moja labandua Gor nje ya Klabu Bingwa Afrika
Na GEOFFREY ANENE
BAO la Anice Badr lilitosha kunyima Gor Mahia karibu Sh56 milioni na tiketi ya mechi za makundi kwenye Klabu Bingwa Afrika nchini Tunisia, Jumapili.
Mvamizi huyu wa Esperance alimwaga kipa Bonface Oluoch katika dakika ya 21 uwanjani Rades katika mchuano huo wa marudiano wa raundi ya kwanza.
Vijana wa kocha Dylan Kerr, ambao walikabwa 0-0 uwanjani Kenyatta mjini Machakos mnamo Machi 7, walihitaji ushindi ama sare ya aina yoyote kusonga mbele.
Hata hivyo, licha ya kujituma vilivyo, Gor haikuweza kulipiza kisasi.
Gor ilibanduliwa tena na Esperance katika raundi ya kwanza kwenye Klabu Bingwa mwaka 2014. Mwaka huo, Esperance ilishinda 3-2 nchini Kenya kabla ya kupepeta Gor 5-0 mjini Rades katika mechi ya marudiano.
Mahasimu hawa waliwahi kukutana katika fainali ya mashindano ya Afrika ya Cup Winner’s Cup mwaka 1987. Gor ilinyakua taji kwa mabao ya ugenini baada ya mikondo yote miwili kumalizika 3-3. Zilitoka sare ya 2-2 nchini Tunisia na 1-1 nchini Kenya.
Zawadi ya kufika mechi za makundi katika makala ya mwaka 2018 ni Sh56 milioni timu ikimaliza katika nafasi mbili za mwisho kwenye kundi lake.
Robo-fainali ina tuzo ya Sh66 milioni na nusu-fainali Sh8 milioni. Bingwa atazawadiwa Sh253.6 milioni naye nambari mbili atatia mfukoni Sh126.8 milioni.
Baada ya kupigwa na Esperance 1-0, Gor sasa imeteremka hadi mashindano ya daraja ya pili ya Afrika (Confederations Cup).
Mabingwa hawa mara 16 wa Kenya watapiga mechi muondoano kati ya Aprili 6 na Aprili 18 ili kuingia mechi za makundi za Confederations Cup. Gor itafahamu mpinzani wake katika mechi za muondoano hapo Machi 21 droo itakapofanywa.
Baadhi ya wapinzani inaweza kukutana nao ni Fosa Juniors (Madagascar) iliyobandua nje mabingwa mara 13 wa Kenya AFC Leopards, Raja Casablanca (Morocco), SuperSport United (Afrika Kusini), Enyimba (Nigeria) na Al-Masry (Misri), miongoni mwa wengine.
Raundi ya muondoano itahusisha klabu 32 (16 zilizopoteza katika raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa na 16 zilizoshinda katika raundi ya kwanza ya Confederations Cup). Washindi katika awamu hii wataingia mechi za makundi.
Timu zitakazomaliza mechi za makundi katika nafasi ya tatu na nne zitazawadiwa Sh27.8 milioni. Robo-fainali na nusu-fainali ina tuzo ya Sh35.5 milioni na Sh45.6 milioni, mtawalia. Bingwa na nambari mbili watapokea Sh126.8 milioni na Sh63.4 milioni, mtawalia.