Bao tamu la Wanyama lachangamsha mitandao
Na GEOFFREY ANENE
VICTOR Wanyama alifunga bao safi na kufungulia timu yake ya Tottenham Hotspur milango ya kuangamiza Huddersfield 4-0 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza nchini Uingereza, Jumamosi.
Nahodha huyu wa Harambee Stars alichenga beki moja na kisha kipa Ben Hamer kabla ya kufunga bao tamu la ufunguzi kupitia mguu wake wa kushoto dakika ya 24 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mhispania Fernando Llorente.
Mbrazil Lucas alifanya mambo kuwa 2-0 dakika tatu baadaye alipomegewa pasi nzuri kutoka kwa Mfaransa Moussa Sissoko.
Lucas alizamisha kabisa chombo cha Huddersfield alipoongeza bao la tatu dakika ya 87 baada ya kumegewa pasi na raia wa Denmark Christian Eriksen na kugonga msumari wa mwisho katika dakika za majeruhi Mkorea Son Heung-min alipompa pasi murwa.
Mchuano huu ulikuwa wa kwanza ligini kwa kiungo Wanyama, 27, kucheza dakika 90 tangu dhidi ya Crystal Palace mnamo Novemba 10 mwaka 2018.
Baada ya mechi ya Palace, Wanyama aliuguza jeraha la goti lililomkosesha mechi 17 mfululizo katika mashindano yote.
Alipata kuanzishwa dhidi ya Huddersfield baada ya kumiminiwa sifa kwa kuonyesha ubabe wake uwanjani dhidi ya Manchester City katika mechi ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya hapo Aprili 9 alipochezeshwa dakika 10 pekee za mwisho.
Baada ya ushindi huu wa pili mfululizo, Spurs sasa imerukia nafasi ya tatu kwenye jedwali kwa alama 67 kutokana na mechi 33 na kusukuma Chelsea nafasi moja chini.
Chelsea ina alama 66. Liverpool inaongoza kwa alama 82 baada ya kucheza mechi 33. City ni ya pili kwa alama 80 kutokana na mechi 32. Spurs, Chelsea, Arsenal na Manchester United zinawania kumaliza ligi ndani ya mduara wa nne-bora ili kufuzu kushiriki Klabu Bingwa msimu ujao.