Michezo

Barca kukutana na Mallorca Juni 13

June 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

BARCELONA watarejelea kampeni za kutetea ufalme wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu dhidi ya Real Mallorca.

Soka ya La Liga iliyositishwa ghafla mnamo Machi 12, 2020 kutokana na janga la corona sasa itaanza upya mnamo Juni 11 na suala hilo limethibitishwa na Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.

Barcelona watasafiri ugenini kwa kivumbi hicho dhidi ya Mallorca mnamo Juni 13, siku mbili baada ya msimu huu wa La Liga kurejelewa rasmi kwa gozi la jiji la Seville kati ya Real Betis na Sevilla.

Hadi kusimamishwa kwa kipute cha La Liga, Barcelona walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 58 kutokana na mechi 27. Real Madrid ambao ni wa pili kwa pointi 56, watajibwaga ugani kwa mchuano wao wa kwanza baada ya janga la corona dhidi ya Eibar mnamo Juni 13.

Waandalizi wa La Liga wamefichua ratiba ya mechi za raundi mbili pekee kati ya 11 zilizosalia muhula huu. Ingawa hivyo, Javier Tebas ambaye ni Afisa Mkuu wa La Liga amesema kwamba mechi zitakuwa zikipigwa kila siku ya wiki hadi msimu huu utakapokamilika rasmi mnamo Julai 19, 2020.

Baada ya kuvaana na Mallorca, Barcelona wamepangiwa kupimana ubabe na Leganes mnamo Juni 16 huku Real wakipepetana na Valencia siku mbili baadaye.

La Liga itakuwa kipute cha pili miongoni mwa Ligi Kuu tano za bara Ulaya kurejelewa baada ya soka ya Ujerumani kuanza upya mnamo Mei 16. Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) imepangiwa kurejelewa Juni 17, siku tatu kabla ya kipenga cha kuashiria kuanza upya kwa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kupulizwa.