Barcelona katika hatari ya kuwa 'AC Milan au Manchester United nyingine'
Na CHRIS ADUNGO
VICTOR Font amesema Barcelona wako katika hatari ya kuandamwa na mikosi iliyowahi kuwapata AC Milan na Manchester United ambao walipungua makali na kushindwa kabisa kuwania mataji ya haiba kubwa katika soka ya bara Ulaya.
Font anapania kumdengua Josep Maria Bartomeu kwenye uchaguzi mkuu wa Barcelona mnamo 2021.
Real Madrid waliwapiga kumbo Barcelona katika hatua za mwisho za kampeni za msimu huu na kutia kapuni ubingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu mnamo Julai 16, 2020.
Kwa mujibu wa Font, Barcelona ni miongoni mwa vikosi vya haiba kubwa zaidi duniani ambavyo kwa sasa viko katika hatari ya kushindwa kabisa kutamba katika soka ya bara Ulaya iliyo na ushindani mkali.
Kulingana naye, Barcelona wana kibarua kikubwa cha kubadilisha kizazi kizima cha wanasoka wao, kuukarabati uwanja wao wa Camp Nou na kukabiliana na athari nyingi za kifedha ambazo zimeachwa na janga la corona.
“Soka imebadilika sana katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na ikawa ya kitaaluma zaidi. Huwezi kabisa kulinganisha soka ya sasa ya La Liga ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambayo inaendeshwa kitaalamu zaidi. Tusipobadilika, Barcelona itakuwa AC Milan na Man-United nyingine,” akasema Font.
AC Milan walinyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa mara ya mwisho mnamo 2010-11 huku Man-United wakitawazwa mabingwa wa taji la EPL kwa mara ya mwisho mnamo 2012-13.
Maoni ya Font yameungwa mkono na nahodha wa Barcelona, Lionel Messi ambaye amesema “italazimu mambo kubadilika” uwanjani Camp Nou ili kukijenga upya kikosi hicho ambacho kwa sasa ni “dhaifu” na “tepetevu”.
Font ambaye ni mfanyabiashara maarufu nchini Uhispania, ndiye mwaniaji wa pekee ambaye amejitokeza kumpinga Bartomeu katika uchaguzi mkuu ujao wa urais wa Barcelona.
Kati ya mipango yake uwanjani Camp Nou ni kumpokeza mikoba ya ukocha kiungo wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez ambaye anapigiwa upatu kumrithi mkufunzi Quique Setien. Xavi, 40, kwa sasa anadhibiti mikoba ya kikosi cha Al-Sadd nchini Qatar.
Matamanio ya Font pia ni kumdumisha Messi kambini mwa Barcelona baada ya kuibuka kwa tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kutua kambini mwa Inter Milan, Juventus au Manchester City baada ya mkataba wake kutamatika rasmi Barcelona mnamo 2021.
Matumaini ya pekee kwa Barcelona kutwaa taji msimu huu sasa yanasalia kwenye kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambapo kwa sasa wanajiandaa kurudiana na Napoli waliowalazimisha sare ya 1-1 nchini Italia katika mkondo wa kwanza.