Bayern Munich imetuaibisha, kutudhalilisha na kutusambaratisha – Barcelona
Na CHRIS ADUNGO
BEKI Gerard Pique, 33, amesema kwamba mabadiliko makubwa muhimu yanahitaji kufanyika kambini mwa Barcelona iwapo miamba hao wa soka ya Uhispania watataka kurejelea uthabiti wao wa zamani.
Chini ya kocha Quique Setien, Barcelona walidhalilishwa na kuaibishwa na Bayern Munich ya Ujerumani kwa kichapo cha mabao 8-2 kwenye robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 14, 2020 jijini Lisbon, Ureno.
Thomas Muller aliyefunga mabao mawili, aliwaweka Bayern kifua mbele kunako dakika ya nne kabla ya David Alaba kujifunga dakika tatu baadaye na kusawazisha mambo. Kufikia mwisho wa kupindi cha kwanza, Bayern walikuwa wakijivunia mabao 4-1 baada ya kufungiwa mengine na Ivan Perisic na Serge Gnabry.
Luis Suarez alifungia Barcelona katika dakika ya 57 kabla ya Bayern kuwashukia zaidi kwa mabao kupitia kwa Joshua Kimmich, Robert Lewandowski na Philippe Coutinho aliyecheka na nyavu mara mbili. Coutinho ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Liverpool, anachezea Bayern kwa mkopo kutoka Barcelona.
Kichapo hicho ndicho kinono zaidi kwa Barcelona ambao ni mabingwa mara tano wa UEFA kuwahi kupokea katika soka ya bara Ulaya.
Ni kichapo ambacho pia kilikamilisha msimu mbaya uliowashuhudia wakiambulia nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kupigwa kumbo na watani wao wa tangu jadi, Real Madrid. Huu ni msimu wa kwanza tangu 2013-14 kwa Barcelona kukamilisha kampeni zao bila kunyanyua taji lolote.
“Tumefika mwisho wa safari na dalili zote zinaashiria kwamba tumesambaratika. Haijakuwa mara ya kwanza, ya pili au ya tatu. Hatujakuwa katika mkondo mzuri na hali hii inatisha na kusikitisha zaidi,” akatanguliza Pique.
“Makocha na wachezaji hupishana katika kila kikosi. Lakini miaka mingi imepita tangu ushawishi wa Barcelona uhisike katika ulingo wa soka ya bara Ulaya.”
“Lazima tujisake upya ndani kwa ndani na kuamua nini kitakachokuwa bora kwa klabu ndipo tujikomboe. Matokeo dhidi ya Bayern hayawezi kustahimilika, hayakubaliki kabisa, yanatia aibu na yanadunisha.”
“Ni vigumu sana kujihusisha na matokeo hayo, ila nina matumaini kwamba yatakuwa kiini cha mwanzo mpya. Mwanzo wa mabadiliko muhimu ambayo yanahitaji kufanyika haraka iwezekanavyo.”
“Klabu inahitaji kusukwa upya na mfumo mzima wa uongozi kuondolewa. Sisemi hivi kwa niaba ya kocha au wachezaji wenzangu. Hizi ni fikira na hisia zangu binafsi. Wakati umefika kwa usimamizi wa Barcelona kufikiria sana na kusikia kilio cha wazalendo kindakindaki wa kikosi hiki na kutilia maanani maoni ya watu wengine ambao wameokana duni machoni pa wengine,” akasema Pique kwa kusisitiza kwamba atakuwa wa kwanza kuagana rasmi na Barcelona iwapo hawatawazia kusajili wanasoka wapya na kuisuka upya kabisa benchi ya kiufundi.
Barcelona walitawazwa mabingwa wa UEFA kwa mara ya mwisho mnamo 2014-15. Wanatarajiwa kuandaa uchaguzi wa urais wa klabu mnamo 2021 ambapo huenda wakapata mrithi wa Josep Maria Bartomeu ambaye amekuwa kinara kambini mwa kikosi hicho cha Camp Nou tangu 2014.
Setien aliwaongoza masogora wake kupepetana na Bayern kwenye robo-fainali za UEFA akiwa tayari na presha tele kutokana na ubovu wa matokeo ya kikosi chake chini yake kipindi cha miezi saba iliyopita.
Mkufunzi huyo wa zamani wa Real Betis aliaminiwa mikoba ya Barcelona mnamo Januari 2020 baada ya kikosi hicho kilichomtimua kocha Ernesto Valverde kumpokeza mkataba wa miaka miwili na nusu.
Kwa mujibu wa Pique, chombo cha Setien ki motoni na kutimuliwa kwake huenda kukampisha kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur Mauricio Pochettino au aliyekuwa mkufunzi wa Everton, Ronald Koeman ambao wamekuwa wakihusishwa pakubwa na mikoba ya Barcelona.
Koeman, ambaye amekuwa kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi tangu 2018, aliwahi kuvalia jezi za Barcelona kwa miaka sita akiwa mchezaji kati ya 1989-1995. Kwa upande wake, Pochettino ambaye ni mzawa wa Argentina na rafiki wa karibu wa Bartomeu, hajawahi kupata klabu ya kunoa tangu atimuliwe na Tottenham mnamo Novemba 2019.
Kichapo ambacho Barcelona walipokezwa na Bayern ndicho kinono zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kupokezwa katika UEFA tangu Valencia wapepetwe na Inter Milan 6-2 mnamo Septemba 1962.
Ni mara yao ya kwanza kuwahi kufungwa mabao manane katika mechi moja tangu wapokezwe na Sevilla kichapo cha 8-0 mnamo Aprili 1946.
Isitoshe, ni mara ya kwanza kwa Barcelona kuwahi kupoteza mechi kwa mabao sita tangu wacharazwe 6-0 na Espanyol mnamo Aprili 1951.