Bayern Munich yafurusha kocha baada ya kichapo wikendi
Na MASHIRIKA
MUNICH, UJERUMANI
BAYERN Munich wameagana rasmi na kocha Niko Kovac, 48.
Uamuzi huo unatokana na tukio la Bayern kupepetwa 5-1 na Eintracht Frankfurt katika mchuano wa Ligi Kuu ya Bundesliga wikendi iliyopita.
Mchuano huo ulikuwa wa pili kwa Bayern kupoteza kutokana na michuano 10 ya hadi kufikia sasa msimu huu ligini.
Ilikuwa baada ya beki wao matata, Jerome Boateng kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya dakika tisa pekee za ufunguzi wa mchuano huo. Filip Kostic na Djibril Sow waliwaweka Frankfurt kifua mbele kabla ya Robert Lewandowski kuwafungia Bayern bao lililopania kuwarejesha mchezoni kunako dakika ya 14.
Kipindi cha pili
David Abraham aliyafanya mambo kuwa 3-1 pindi baada ya kipindi cha pili kuanza kabla ya mabao mengine kupachikwa wavuni kupitia kwa Martin Hinteregger na Goncalo Paciencia.
Ushindi mnono wa 8-0 uliovunwa na RB Leipzig dhidi ya Mainz na ule wa 3-0 uliosajiliwa na Borussia Dortmund dhidi ya VfL Wolfsburg uliwasaza Bayern katika nafasi ya nne. Adhabu ambayo Bayern walipokezwa ilikuwa zao la Boateng kumchezea visivyo Paciencia aliyeongoza mashambulizi ya Frankfurt kwa kushtukiza.
Kovac anabanduka kambini mwa Bayern kikosi hicho kikishikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 19, tatu nyuma ya viongozi Borussia Monchengladbach.
Kocha huyo ambaye ni kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Croatia amekuwa akidhibiti mikoba ya Bayern tangu Julai 2018. Hadi kutimuliwa kwake, alikuwa amewaongoza miamba hao wa Ujerumani kutia kapuni mataji mawili katika kampeni za msimu uliopita.
Katika jumla ya mechi 65 alizosimamia kambini mwa Bayern, Kovac aliwaongoza miamba hao kusajili ushindi mara 45. Kichapo cha 5-1 kutoka kwa Frankfurt wikendi iliyopita ndicho kinono zaidi kwa Bayern kuwahi kupokezwa ligini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
“Kufutwa kwa Kovac ni maamuzi yaliyofikiwa na usimamizi wa Bayern baada ya kushauriana kwa kina na kocha huyo mnamo Jumapili. Matokeo duni ambayo yamesajiliwa na kikosi katika mechi za hivi karibuni ni jambo ambalo lilituweka katika ulazima wa kuichukua hatua hiyo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge katika taarifa yake.
Majadiliano
“Tulijadiliana na Kovac kwa uwazi baada ya kuandaa kikao cha dharura pamoja na wachezaji wote. Usimamizi uliamua kumfuta kazi kutokana na msururu wa matokeo duni ambayo yamesajiliwa na kikosi hadi kufikia sasa muhula huu,” akaongeza Rummenigge.
Katika kipindi cha miezi 18 ambayo Kovac ameshikilia mikoba ya Bayern, kikosi hicho kimenyanyua ubingwa wa Bundesliga mara moja, DFB Cup na Supercup.
Aliyekuwa msaidizi wa Kovac, Hansi Flick atasimamia mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) utakaowakutanisha Bayern na Olympiakos hapo kesho kabla ya kukiongoza kikosi hicho kuvaana na Borussia Dortmund katika gozi kali la Bundesliga litakalowakutanisha ugani Signal Iduna Park mwishoni mwa wiki hii.