Michezo

Bayern Munich yapiga PSG 1-0 na kutwaa ufalme wa UEFA

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich walilemea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa bao 1-0 kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu iliyochezewa jijini Lisbon, Ureno mnamo Jumapili, Agosti 23, 2020.

Fowadi mzawa wa Ufaransa Kingsley Coman, 24, aliyepokezwa malezi ya kusakata soka kambini mwa PSG, ndiye alifunga bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo.

Goli hilo la dakika ya 59 lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya nyota huyo wa zamani wa Juventus na Joshua Kimmich.

Ilikuwa fahari na tija kubwa zaidi kwa Hansi Flick ambaye sasa amewaongoza Bayern kunyanyua mataji matatu katika msimu wake wa kwanza akiwa kocha mkuu.

Hadi walipowalaza PSG, Bayern walikuwa wametia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na ufalme wa German Cup katika kampeni za msimu huu wa 2019-20.

Flick, aliyekuwa kocha msaidizi wa Bayern, aliaminiwa na waajiri kuwa mrithi wa mkufunzi Niko Kovac ambaye alitimuliwa Novemba 2019 kutokana na matokeo duni.

Kwa upande mwingine, ilikuwa fadhaa kwa nyota Neymar Jr na Kylian Mbappe ambao walishindwa kutambisha PSG licha ya ukubwa wa uwezo wao kila wanapokuwa uwanjani.

Badala yake, walisalia wanyonge na juhudi zao langoni pa Bayern zikazimwa kirahisi na kipa na nahodha wa Bayern, Manuel Neuer.

Mbappe na Neymar walipoteza nafasi mbili za wazi za kufungia PSG mabao muhimu katika kipindi cha kwanza na pili.

Bayern ambao kwa sasa ni mabingwa mara sita wa taji la UEFA, ni kikosi cha kwanza kutawala soka ya bara Ulaya baada ya kushinda kila mchuano katika kampeni za msimu huu.

Chini ya Flick, Bayern pia wanajivunia rekodi ya kutoshindwa hadi kufikia sasa mwaka huu wa 2020, na hawajapoteza mechi yoyote kati ya 21 zilizopita.

Mojawapo ya mabadiliko muhimu yaliyomvunia Flick ufanisi mkubwa dhidi ya PSG ni kumwajibisha Coman katika kikosi cha kwanza badala ya Ivan Perisic wa Croatia.

Kikosi hicho kinatazamiwa kuimarika hata zaidi msimu ujao baada ya kusajiliwa kwa aliyekuwa kiungo wa Manchester City, Leroy Sane.

Msimu huu umekuwa bora zaidi kwa PSG katika kivumbi cha UEFA ambacho kimewashuhudia wakitinga fainali kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 27.

Kibarua zaidi kwa miamba hao wa Ufaransa na kocha Thomas Tuchel ni jinsi ya kujinyanyua haraka na kujisuka upya hasa ikizingatiwa kwamba wataagana rasmi na nahodha beki tegemeo mzawa wa Brazil, Thiago Silva.

Bayern wamenyanyua kwa sasa taji la UEFA mara sita (sawa na Liverpool) na msimu huu ulikuwa wao wa kwanza kutia kapuni taji hilo tangu 2012-13. Ni Real Madrid (mara 13) na AC Milan (mara saba) ndio wanaojivunia rekodi ya kutawazwa mabingwa wa UEFA mara nyingi zaidi.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa PSG kushindwa kufunga bao kwenye mechi ya bara Ulaya baada ya michuano 35. Mara ya mwisho kwa kikosi hicho kutofunga goli ni wakati walipocharazwa 1-0 na Manchester City mnamo Aprili 2016.

Timu zote ambazo zimekuwa zikiwania ubingwa wa UEFA kwa mara ya kwanza katika hatua ya fainali zimepoteza na kikosi cha pekee kilichowahi kufaulu ni Borussia Dortmund ya Ujerumani iliyowaangusha Juventus kutoka Italia mnamo 1997.

Ni mara nne pekee katika historia ambapo kocha anayemzidi Flick kiumri (miaka 55 na siku 181) amewahi kutwaa ufalme wa UEFA. Hao ni Goethals aliyeongoza Olympique Marseille kutawazwa mabingwa mnamo 1993 akiwa na umri wa miaka 71, Heynckes wa Bayern mnamo 2013 akiwa na miaka 68 na Alex Ferguson akiwa Man-United mnamo 1999 na 2008 akiwa na umri wa miaka 57 na 66 mtawalia.

Bayern ndicho kikosi cha tatu katika historia kuwahi kufunga mabao 500 kwenye UEFA baada ya Barcelona (517) na Real Madrid (567).

Coman ndiye Mfaransa wa tano kuwahi kufunga bao kwenye fainali ya UEFA baada ya Karim Benzema 2018, Zinedine Zidane 2002, Desailly 1994 na Boli mnamo 1993.

Kipa Keylor Navas aliyesajiliwa na PSG kutoka Real, ni mlinda-lango wa tatu kuwahi kucheza fainali ya UEFA akivalia jezi za vikosi viwili baada ya Hans-Jong Butt (Bayern na Bayer Leverkusen) na Edwin van der Sar (Man-United na Ajax Amsterdam).

Bayern walijibwaga ugani kwa fainali dhidi ya PSG wakijivunia motisha tele baada ya kuwadengua Barcelona kwa mabao 8-2 kwenye robo-fainali kabla ya kucharaza Olympique Lyon ya Ufaransa 3-0 kwenye nusu-fainali. Awali walikuwa wamewabandua Chelsea kwa kichapo cha 7-1 katika hatua ya 16-bora.

Kwa kutwaa ufalme, Bayern walikomesha nuksi ya misimu minne iliyopita ambayo imewashuhudia wakibanduliwa kwenye kipute cha UEFA katika hatua ya nusu-fainali.

PSG ambao ni mabingwa wa Ligue 1, French Cup na French League Cup, walifuzu kwa fainali ya UEFA baada ya kuwapokeza Borussia Dortmund kichapo cha 3-2 kwenye hatua ya 16-bora kabla ya kutoka nyuma na kubandua Atalanta ya Italia kwenye robo-fainali.

Ufanisi huo wa PSG uliwakatia tiketi ya nusu-fainali za UEFA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 27 na wakafaulu kuwapepeta RB Leipzig ya Ujerumani 3-0.

Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, PSG wamekuwa na nuksi ya kuaga mapema kivumbi cha UEFA ambapo wameondolewa kwenye hatua ya 16-bora.

Kabla ya hapo, walikuwa wamebanduliwa kwenye hatua ya robo-fainali katika kipindi cha miaka minne mfululizo. Matokeo hayo duni yalikuwa kiini cha kutimuliwa kwa waliokuwa wakufunzi wao Laurent Blanc na Unai Emery.