Bei ghali ya Wanyama yafukuza wanunuzi
Na MWANDISHI WETU
TOTTENHAM Hotspur italazimika kupunguza bei ya Victor Wanyama ili kuvutia wateja kabla ya soko kufungwa Januari 31 baada ya tetesi nchini Uingereza kudai kuwa klabu haziko tayari kutoa Sh1.1 bilioni zinazoitishwa.
Ripoti kutoka jijini London zinasema kuwa klabu hiyo inatatizika kupata mnunuzi wa kiungo huyo, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.
Fununu zinasema Wanyama anamezewa mate na miamba wa Italia AC Milan pamoja na Norwich na Aston Villa iliyonyakua Mtanzania Mbwana Samatta mapema juma hili kutoka Ubelgiji na pia mabingwa wa Uturuki, Galatasaray. Alihusishwa pia na West Ham na miamba wa Scotland, Celtic.
Spurs ilitangaza bei ya Wanyama kuwa Sh2.2 bilioni mwisho wa msimu uliopita kabla ya kukubali kumuuza kwa Club Brugge nchini Ubelgiji. Hata hivyo, ripoti zinadai mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikataa kurejea Ubelgiji alikoanzia soka yake ya watu wazima mwaka 2008.
Miezi mitano baada ya uhamisho huo kugonga mwamba, Wanyama anasalia na miezi 18 katika kandarasi yake na sasa bei ya kwanza ya Spurs inakaribia kufika nusu. Kuna uwezekano mkubwa itapunguka hata zaidi.
Makombo
Wanyama anaonwa na Tottenham kuwa makombo, huku akitumiwa mara moja tu na kocha mpya Jose Mourinho katika mechi ambayo haikuwa na umuhimu mkubwa ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Wajerumani Bayern Munich mwezi uliopita.
Taarifa zinasema klabu kadhaa zimeulizia huduma za Wanyama zikiwemo mbili kutoka Ligi Kuu ya Uingereza, lakini hakuna hata moja iliyo tayari kutoa fedha Spurs inazoitisha. Inaaminika mshahara wa Wanyama wa Sh8.2 milioni kila wiki pia ni kizingiti kikubwa.
Mkenya huyo alijiunga na Tottenham jijini London kwa Sh1.4 bilioni kutoka Southampton mwaka 2016 akifuata kocha Mauricio Pochettino, ambaye pia alimleta nchini Uingereza kutoka Celtic mwaka 2013.
Aling’ara katika msimu wake wa kwanza Tottenham na hata kutajwa mmoja wa viungo bora duniani, lakini majeraha yamemsumbua tangu msimu 2017-2018 na kupoteza nafasi yake timuni.