Bendtner akiri alipata funzo la mwaka kupoteza Sh700m katika kamari
Na GEOFFREY ANENE
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Arsenal, Nicklas Bendtner amesimulia jinsi alivyopata funzo kali katika mchezo wa karata alipopoteza Sh698,701,057 akiwa na umri wa miaka 19.
Bendtner, 32, ambaye sasa hana klabu, alijiunga na Arsenal akiwa na umri wa miaka 16 mwaka 2004 na kuchezea timu ya watu wazima kati ya mwaka 2005 na 2014 na pia Birmingham City, Sunderland na Juventus kwa mkopo kabla ya kuyoyomea Wolsfburg, Rosenborg na FC Copenhagen.
Akizungumza katika kipindi cha runinga cha Bendtner & Philine nchini mwake Denmark anachofanya na mpenzi wake Philine Roepstorff, Bendtner alisema alitumia mshahara wake mwingi kwenye mchezo wa karata wa Texas Hold’Em.
“Ni vigumu kusema kiasi kamili cha fedha nilichopoteza, lakini ni kikubwa. Nakisia ni karibu Korona 50 milioni (pauni 5.4 milioni za Uingereza). Ni tabia ambayo nilikuwa naweza kudhibiti na nilikuwa nawekeza fedha nyingi. Hata hivyo, wakati mmoja mjini London mambo karibu yaharibike kabisa. Kwa sasa, mimi huwekeza fedha ndogo kama Korona 100 (Sh1,555),” alinukuliwa na vyombo vya habari akisema.