Brazil wanyanyua taji la Copa America
Na MASHIRIKA
RIO DE JANEIRO, BRAZIL
FOWADI Gabriel Jesus wa Manchester City alifunga bao na kuchangia jingine kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika ushindi uliowavunia Brazil ubingwa wa taji la Copa America baada ya kuwakomoa Peru 3-1 jijini Rio de Janeiro mnamo Jumapili.
Krosi ya Jesus ilijazwa kimiani na nyota Everton Sousa Soares kunako dakika ya 15 kabla ya Paolo Guerrero kuwarejesha Peru mchezoni kwa kusawazisha kunako dakika ya 44.
Ingawa hivyo, Jesus alikiyumbisha zaidi mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 70. Richarlson Andrade wa Everton aliwafungia Brazil bao la tatu kupitia mkwaju wa penalti mwishoni mwa kipindi cha pili.
Ushindi kwa Brazil ulimpa Jesus kitulizo kamili hasa ikizingatiwa kwamba alianza kutiririkwa na machozi alipofurushwa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu. Aidha, akitoka uwanjani, nyota huyo alipiga teke chupa ya maji kabla ya kusukumu mtambo wa VAR uliorejelewa na refa kabla ya kumlisha kadi ya pili ya manjano.
Ilikuwa ni mara ya tisa kwa Brazil kutwaa ubingwa wa Copa America na ushindi huo ulikuwa wao wa kwanza tangu watie kapuni nishani ya dhahabu katika Olimpiki za Rio de Janeiro mnamo 2016.
Ushindi pia uliwapa Brazil fursa ya kuendeleza rekodi yao ya kushinda ubingwa wa Copa America kila mara ambapo wamekuwa wenyeji wa fainali hizo.
Gabriel apata fursa kudhihirisha uwezo wake
Kipindi cha kwanza cha fainali kati ya Brazil na Peru kilitoa jukwaa mwafaka zaidi kwa Jesus kutamba baada ya kukosolewa pakubwa na mashabiki wa timu ya taifa katika kampeni za awali.
Fowadi huyo alishindwa kabisa kufunga bao katika jumla ya mechi tano zilizopigwa na Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Urusi mwaka 2018.
Brazil walishuka dimbani wakijivunia hamasa ya kuwachabanga Argentina 2-0 katika nusu-fainali. Kwa upande wao, Peru walitarajiwa kuchuma nafuu kutokana na ufanisi wa kuwabandua Chile ambao walitawazwa mabingwa wa 2015 na 2016.
Argentina walikamilisha kampeni za Copa America mwaka huu katika nafasi ya tatu huku Chile waliokuwa mabingwa watetezi wakiridhika na nafasi ya nne.
Kikubwa zaidi kilichotarajiwa kuwaaminisha Brazil kabla ya kuchuana na Peru ni ushindi mnono waliousajili dhidi ya kikosi hicho katika mchuano wa makundi uliowakutanisha kwenye fainali za mwaka huu. Katika mchuano huo wa mwisho wa Kundi A, Brazil walivuna ushindi mnono wa 5-0 siku saba baada ya kuwalaza Bolivia 3-0 katika mechi ya ufunguzi kisha kuambulia sare tasa na Venezuela.